1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon: Hezbollah yashambulia maeneo ya kijeshi ya Israel

Hawa Bihoga
9 Oktoba 2024

Wanamgambo wa Hezbollah wameshambulia kwa makombora wanajeshi wa Israel karibu na kijiji cha mpakani nchini Lebanon ikiwa ni siku moja baada ya Israel kutangaza kuwa limewauwa warithi wawili wa kiongozi wake alieuwawa.

Libanon | Luftangriffe in Beirut
Picha: AFP/Getty Images

Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran ambalo limekuwa likivurumisha makombora dhidi ya Israel kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kile ilichokisema ni kuunga mkono washirika wake Hamas, ambayo kwa sasa inakabiliana na oparesheni ya Israel ya ardhini, limesema kwamba mashambulizi yake ya leo Jumatano yamewarudisha nyuma wanajeshi wa Israel.

Jeshi la Israel katika taarifa yake limesema wanajeshi wake watatu walijeruhiwa vibaya hapo jana Jumanne na leo Jumatano wakati wa mapigano kusini mwa Lebanon.

Mapema siku ya Jumatano ving'ora vya tahadhari vimelia kaskazini mwa Israel, baada ya Israel kufanya mashambulizi mapya ya mabomu usiku kucha katika vitongoji vya kusini mwa Beirut ambayo ni ngome ya Hezbollah.

Soma pia:Israel yaingia kijeshi Lebanon "kuisambaratisha Hezbollah"

Mzozo nchini humo umeendelea kuongezeka katika wiki za hivi karibuni huku Israel ikifanya mkururo wa mauaji ya viongozi wa ngazi za juu wa kundi la Hezbollah na kuanzisha oparesheni za ardhini kusini mwa Lebanon.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Hezbollah yameua zaidi ya watu 2,100, vifo vingi vikiwa ni katika wiki mbili zilizopita na kuwalazimisha watu milioni 1.2 kuyakimbia makaazi yao. Mohammad ni raia wa Lebanon aliekimbia mapigano anasema hali kusini mwa taifa lale ni ya kutisha.

"Hali katika eneo la kusini mwa Lebanon ni ya kutisha. Maeneo mengi yameharibiwa vibaya na hayafai tena kwa kuishi. Nimewaleta watoto wangu hapa kukimbia mabomu." Alisema Mohammed akiwa njiani kuelekea Syria.

Israel kujibu shambulio la Iran?

Kwa mujibu wa chanzo cha karibu kinachofahamu kwa ukaribu mzozo huo kimesema, rais Joe Biden wa Marekani anatarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, baadae siku ya Jumatano. Mazungumzo hayo yanatarajiwa pia kujumuisha mjadala wa mipango mipana ya kuishambulia Iran.

Israel yashambulia katikati mwa Beirut

01:03

This browser does not support the video element.

Eneo la mashariki ya Kati limeendelea kuwa na hofu ikisubiri jibu la Israel baada ya shambulio la Iran wiki iliopita ambalo Tehran ilifanya kulipiza kisasi kwa kuongezeka kwa jeshi la Israeli nchini Lebanon.

Soma pia:Volker Turk azitaka nchi kuchukua hatua dhidi ya Israel

Kwingineko madaktari wa Palestina wamesema takriban watu 18 wameuwawa katika mashambulizi ya Israel, kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia ilioko kaskazini mwa Gaza.

Jeshi la Israel linasema uvamizi huo, ambao sasa umeingia siku ya tano, unanuiwa kuwazuia wapiganaji wa Hamas kufanya mashambulizi zaidi kutoka upande wa Jabalia na kuwazuia kujipanga upya.

Jeshi la Israel kwa mara kadhaa limerudia kutoa indhari ya kuhama kwa wakaazi wa Jabalia na maeneo ya karibu, lakini maafisa wa Palestina na Umoja wa Mataifa wanasema hakuna maeneo salama ya kukimbilia Ukanda wa Gaza.