1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon katika hali ya tahadhari ikihofia kisasi cha Israel

30 Julai 2024

Lebanon iko katika hali ya tahadhari baada ya Israel kuapa kuwa itajibu vikali shambulizi la roketi la Jumamosi kwenye milima ya Golan lililopelekea vifo vya watu 12.

Eneo la Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut ambako safari za ndege zilivugwa
Eneo la Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut ambako safari za ndege zilivugwaPicha: Mohamed Azakir/REUTERS

Alipotembelea siku ya Jumatatu mji wa Majdal Shams uliopo katika eneo la milima ya Golan kulikotokea shambulizi la roketi lililowaua vijana 12 siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliapa kulipiza kisasi kwa hatua kali, huku wanadiplomasia wakitoa miito ya kuchukua hatua za kuzuia kuongezeka kwa uhasama kati ya Israel na kundi la Hezbollah.

Israel na Marekani zilidai kuwa shambulio hilo liliendeshwa na kundi la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran, ambalo limekuwa likishambuliana karibu kila siku na wanajeshi wa Israel tangu vilipoanza vita vya Gaza kati ya Hamas na Israel Oktoba 7 mwaka jana.

Soma pia: Israel yaapa kulipiza kisasi baada ya vijana 12 kuuawa

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema vita kati ya Israel na Hezbollah haviepukiki, lakini akasisitiza kuwa Washington ingependelea kuona mzozo huo ukitatuliwa kwa njia ya kidiplomasia. Israel imekuwa ikisisitiza kuwa wanalenga kuiadhibu Hezbollah bila kulitumbukiza eneo hilo kwenye vita kamili.

Wanajeshi wa Israel wakiwa kwenye luteka ya kijeshi katika eneo la milima ya GolanPicha: Ronen Zvulun/REUTERS

Hata hivyo viongozi wa eneo la milima ya Golan iliyonyakuliwa na Israel kutoka Syria mwaka 1967 wamesema wanajitenga na uamuzi wa Israel. Wakaazi wengi wa Majdal Shams walikataa hadi leo hii kuchukua uraia wa Israel.

Soma pia: Ujerumani yatoa mwito wa kufanyika juhudi kuzuia mgogoro kamili kati ya Israel na Lebanon

Hezbollah hata hivyo imekanusha kuhusika na shambulio hilo la Jumamosi lakini imechukua tahadhari ya kuhamisha vituo vyake kutoka kusini na mashariki mwa Lebanon. Pia hali ya taharuki ilivuruga safari za ndege katika uwanja wa kimataifa wa Beirut.

Kauli za viongozi mbalimbali ndani na nje ya Lebanon

Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon Abdallah Bou Habib amesema msururu wa harakati za kidiplomasia zimefanyika ili kuzuia makali ya majibu yanaotarajiwa ya Israel, na kwamba pande zote zimeahidi kutoa majibu ya wastani katika mzozo huo. 

Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati amesema mazungumzo yanaendelea katika ngazi za kimataifa kwa kuijumuisha Ulaya, nchi za Kiarabu ili kuilinda Lebanon na kuepusha hali ya hatari.

Rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian (Kulia) akiwa na Kiongozi Mkuu wa Iran Ali KhameneiPicha: leader.ir

Rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian, ambaye nchi yake ndio inaunga mkono Hezbollah na Hamas, ameionya Israel dhidi ya kuishambulia Lebanon, na akasema hilo litakuwa "kosa kuu lenye matokeo makubwa".

Soma pia: UN: Asilimia 80 ya raia wa Gaza wamekimbia makaazi yao

Hayo yakiarifiwa hali bado ni mbaya huko Gaza ambako mashambulizi ya Israel yanaendelea. Sigrid Kaag, Mratibu Mkuu wa masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa na anayehusika kufuatilia Ujenzi mpya wa Gaza amesema:

"Hali bado ni janga kabisa. Kwa muda wa miezi kumi sasa, raia wa Palestina wamekumbwa na msukosuko wa kutisha wa masaibu ya kibinadamu, kuanzia kiwango cha uharibifu hadi athari na kiwewe kwa maisha ya mtu binafsi, bila shaka, hii ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya raia ambao wamepoteza maisha."

Wizara ya afya inayodhibitiwa na  Hamas imesema idadi ya vifo sasa imefikia 39,363. Israel na Hamas wametupiana tena lawama za kukwamisha makubaliano ya usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW