1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon: Miaka 30 baada ya mauaji ya Sabra na Shatila

17 Septemba 2012

Kilomita chache kutoka mahala ambapo jana (16.09.2012) Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 aliongoza misa katika mji wa Beirut, Lebanon, Wapalastina wengi waliukumbuka mwaka wa 30 tangu kutokea mauaji ya Sabra na Shatila.

Mauaji hayo yalichukuwa maisha ya baina watu 800 na 4,000, wakiwemo wanawake na watoto. Wanajeshi wa Israel, ambao waliiteka sehemu ya magharibi ya Beirut, waliizingira kambi ya Wapalastina ya Shatila na baadae ile ya jirani ya Sabra. Wanamgambo wa Kikristo wa Lebanon waliingia na kukaa katika kambi hizo kwa siku tatu na kuwauwa watu wasiokuwa na silaha. Miaka 30 tangu kutokea mkasa huo, jamaa wa watu waliouwawa hawana matumaini zaidi kwamba watu waliofanya kitendo hicho watafikishwa mahakamani.

Katika ziara yake ya punde hivi nchini Lebanon, Baba Mtakatifu alitoa risala ya kutaka kuweko amani katika eneo zima la Mashariki. Vivyo hivyo alifanya mwaka 2009 pale alipotoa ombi la kutambuliwa haki ya Israel ya kuishi kama dola na pia haki ya Wapalastina kuwa na dola yao huru. Lakini kwa Wapalastina wengi ambao ndugu na jamaa zao waliuliwa na wanamgambo wa kikristo katika kambi za Sabra na Shatila, wao walisema kabla ya kuwasili Baba Mtakatifu mjini Beirut kwamba dua kutoka kwa Baba Mtakatifu kwa watu hao waliouliwa ingepunguza maumivu walio nayo.

Mauaji Sabra und Schatila BeirutPicha: Mona Naggar

Haki ya Israel ya kuishi kama dola, na kutambuliwa dola huru ya Wapalastina, mambo hayo yote mawili ni muhimu kwa watu wanaoishi kama wakimbizi kwa sasa zaidi ya miongo mitatu. Wapalastina wengi hawajali kama risala na dua ya aina hiyo ikitoka kwa kiongozi wa dini ambayo sio yao.

Wanamgambo wa kikristo wa Phalangist wa huko Lebanon, wakisaidiwa na wanajeshi wa Israel, wakati Israel ilipouvamia mji wa Beirut mwaka 1982, walizizingira kambi hizo za Wapalastina katika viunga vya mji mkuu huo kabla ya kuingia humo Septemba 16 mwaka 1982. Wanamgambo hao waliingia na kuwauwa wakaazi, wengi wao wakiwa ni Wapalastina. Kuna hadithi kwamba idadi ya watu waliouliwa ilifikia 2,500. Mauaji hayo yalikuwa yanatokana na kilichotajwa kuwa ni kulipiza kisasi kwa kuuliwa rais mteule aliye mkristo, Bashir Gemayel. Aliuliwa kabla ya kuapishwa kukamata madaraka.

Wanaume katika kambi hizo za Sabra na Shatila waliwekwa katika mistari na kuuliwa, wanawake wakabakwa na maiti zikapasuliwapasuliwa na kutupwa majiani. Watu walichinjwa kwa kutumia mashoka na visu. Hii ni kwa mujibu wa watu walionusurika katika mkasa huo. Umm Umar, sasa mwenye umri wa miaka 63, hawezi kujizuia kulia, licha ya kwamba jambo hilo limetokea miaka 30 iliopita. Mpalastina huyo alikuwa anaishi katika mtaa wa Bir Hassan, karibu na kambi ya Wapalastina ya Shatila. Siku ya mauaji hayo, yeye na familia yake wakiwa njiani. Anasimulia hivi:

" Majirani zetu walituambia kwamba inabidi tuende tukapige mhuri vitambulisho vyetu. Kwa hivyo tulielekea ubalozi wa Kuwait. Njiani kote walikuwa wanajeshi wa Israel. Tulisonga mbele na katika njia panda ya Shatila tukakutana na jeshi la wanamgambo wa Lebanon. Jirani zetu walikuwa pia pamoja nasi, Wapalastina, Wasyria na Walibanon. Wanajeshi walitugawa, sisi wakatuweka mbali na wanaume na wakutagawa kwa mujibu wa uraia, Wapalstina na Wasyria upande mmoja, na Walebanon upande mwingine. Sisi wanawake na watoto ilibidi tuelekee katika uwanja wa mpira."

Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 akiongoza Misa Beirut,LibanonPicha: Reuters

Watoto wake wawili, wenye umri wa miaka 15 na 19, pamoja na ndugu yake hajawaona tena, wala maiti zao hazijapatikana. Licha ya Shirika la Msalaba Mwekundu na wakuu wa Lebanon kuulizwa juu ya yale yaliowafika watu hao, lakini hakuna majibu.

Pia kuna mkasa wa Shahira Abudin, ambaye amepoteza jamaa zake saba kutokana na mauaji hayo, wakiwemo baba, mumewe, kaka na dada yake. pamoja na watoto, mdogo kabisa alikuwa ana umri wa miaka miwili. Wao walitafuta hifadhi katika chumba cha nyumba ya shangazi yake huko Shatila. Nje alisikia milio ya risasi na vilio. Punde walifika wanajeshi waliokuwa wanazungumza kiarabu kwa lahaja ya Kilebanon, anakumbuka Shahira Abudin. Anakumbuka walikuwa wanajeshi 16 au 17 hivi. Waliwagawa wanaume na wanawake, na wakawaelekeza wanaume watizame ukuta halafu wakawafyetulia risasi kutoka bunduki za Kalaschnikow. Wanawake na watoto wakafukuzwa, walinusurika na na wao kuuliwa pale afisa mmoja wa jeshi alipingilia kati. Wanawake na watoto waliporejea walikuta nyumba yao imebomolewa kabisa.

Lengo la jeshi la Israel kuingia Lebanon mwaka 1982 lilikuwa kuuteka mji mkuu wa Beirut na kukiangamiza kabisa chama cha ukombozi wa Palastina, PLO, chini ya uongozi wa Yassir Arafat, ambacho kilikuwa kinafyetua maroketi kutokea Lebanon na kuangukia Kaskazini ya Israel. Mwisho wa Agosti, ilibidi Wapalastina wote waliokuwa na silaha waondoke Beirut. Septemba 14, rais-mteule wa Lebanon, Bashir Gemayel aliuliwa kutokana na shambulio la bomu. Yeye alikuwa kiongozi wa wanamgambo wa kikristo wa Lebanon. Wafuasi wake waliwalaumu Wapalastina kwa kuuliwa kiongozi huyo.

Bashir Gemayel aliuliwa kabla ya kukamata madarakaPicha: picture-alliance/ dpa

Hivi sasa kambi ya Shatila ni kama zilivyo kambi nyingine za Wapalastina katika lebanon. Katika barabara zake nyembamba kuna maduka madogomadogo mengi ya kuuza vyakula, mapikipiki na vitu vingine, huku barabara zikijaa taka zenye kunuka. Kuna ubao uliowekwa katika uwanja mwishoni mwa barabara moja ulioandikwa namna hivi: Mashahidi wa Sabra na Shatila". Katika eneo hilo kuna watu waliouliwa Sabra na Shatila ambao wamezikwa hapo.

Shahira Abudin haaminishi hadi leo kwenda katika maeneo ya Wakristo ya Beirut, lakini yeye anasema dhamana ya mauaji hayo ilikuwa ni Israel. Hata hivyo, familia yake haina tamaa ya haki kutendekea. Mwaka 2001, baadhi ya wapalastina walifikisha mashtaka mbele ya mahakama ya Ubelgiji dhidi ya baadhi ya raia wa Israel na wa Lebanon kwa mauaji hayo; pia waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon, alikuwemo kati ya watu waliotakiwa kushtakiwa. Yeye alikuwa waziri wa ulinzi wa Israel wakati wa mauaji. Lakini kesi hiyo iligonga mwamba kwa vile mahakama ya Ubelgiji ilikuwa haiwezi kuwashtaki watu wasiokuweko Ubelgiji. Pia huko Lebanon, wanamgambo wa kikristo walioshiriki katika mauaji hayo hawajashtakiwa hadi leo.

Mwandishi: Naggar, Mona ( ZR): Miraji Othman

Mhariri: Mohammed Abdulrahman