Lebanon na Israel kujadiliana kuhusu mpaka wa baharini
13 Oktoba 2020Eneo hilo linalogombaniwa lina uwezekano wa kuwa na hifadhi kubwa ya nishati ya gesi.
Mazungumzo hayo ambayo Marekani ndio mpatanishi yanafuatia miaka mitatu ya diplomasia ya kina inayofanywa na Marekani na yametangazwa chini ya mwezi mmoja baada ya Marekani kuongeza shinikizo dhidi ya washirika wa kisiasa wa kundi la Lebanon la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Mazungumzo hayo pia yanakuja baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain kukubali kurejesha uhusiano kamili na Israel, chini ya makubaliano ya upatanishi wa Marekani, ambayo yamewavuta baadhi ya washirika wa karibu wa Marekani katika mashariki ya kati kujiweka kando na Iran.
Hezbollah , ambayo ilipigana vita vya wiki tano na Israel mwaka 2006, imesema mazungumzo hayo si ishara ya kuleta amani na adui wake huyo wa muda mrefu. Waziri wa nishati wa Israel pia amesema matarajio katika mazungumzo ya kesho Jumatano ni lazima yaangalie hali halisi.
Majadiliano ya amani
"Hatuzungumzi juu ya majadiliano ya amani na kurejesha uhusiano, badala yake ni jaribio la kutatua mzozo wa kiufundi na kiuchumi ambao kwa miaka kumi umechelewesha hatua za maendeleo za maliasili ya baharini," waziri Yuval Steinitz ameandika katika ukurasa wa Twitter. Spika wa bunge la Lebanon Nabih Berri amesema juhudi za Marekani ni muhimu kwa ajili ya mazungumzo hayo.
"Marekani ina nia ya kuweka juhudi zake zote na pande hizo mbili kusaidia kujenga hali bora na yenye uwezo wa kuleta mafanikio kati ya pande hizo mbili ili kulinda mazungumzo na kuyafikisha mwisho kwa mafanikio haraka iwezekanavyo."
Hata hivyo, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo ameueleza uamuzi huo wa kuendelea na mazungumzo hayo kuwa ni wa kihistoria, na kusema Marekani ina matumaini makubwa kwa mazungumzo tofauti baadaye kuhusiana na kutokubaliana juu ya mpaka wa ardhini wa nchi hizo mbili.
Mkutano wa kesho Jumatano utasimamiwa na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa UNIFIL, ambao umekuwa ukiangalia mzozo huo wa mpaka wa ardhini tangu kuondoka kwa jeshi la Israel kutoka Lebanon kusini mwaka 2000, na kufikisha mwisho miaka 22 ya kulikalia eneo hilo.
Chanzo katika kitengo cha usalama nchini Lebanon kimesema pande hizo mbili zitakutana katika chumba hicho hicho katika kituo cha UNIFIL kusini mwa Lebanon , lakini watafanya mazungumzo yao kupitia mpatanishi.