1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon: Uchunguzi kubaini iwapo mkono wa nje ulihusika

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
7 Agosti 2020

Rais wa Lebanon asema uchunguzi juu ya mlipuko mkubwa mjini Beirut unalenga kubaini iwapo kuna mkono wa nje. Wakati huo huo mashirika ya kimataifa yanaendelea kutafuta misaada kwa ajili ya kuisaidia Lebanon.

Libanon | Nach der schweren Explosion in Beirut | Präsident Michel Aoun
Picha: picture-alliance/dpa/Dalati & Nohra

Wakati ambapo raia wa Lebanon wanajaribu kujenga upya maisha yao juhudi zinaendelea za kuitafuta miili ya watu iliyofunikwa kwenye kifusi baada ya kutokea mlipuko mkubwa katika mji wa Beirut mnamo siku ya Jumanne.

Rais wa Lebanon Michel Aoun amesema uchunguzi unafanyika katika ngazi tatu. Kwanza kubaini jinsi vifaa vya kulipuka vilivyoingia na kuhifadhiwa mahala ambapo mlipuko huo ulipotokea, pili ikiwa mlipuko huo uilisababishwa na uzembe, au ajali na tatu juu ya uwezekano kwamba mkono wa nje umehusika.

Rais wa baraza la Ulaya, ambalo linawakilisha viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya, Charles Michel, anatarajiwa kuwasili mjini Beirut siku ya Jumamosi wakati ambapo jumuia ya Umoja wa Ulaya inajiandaa kuungana pamoja katika juhudi za kuisaidia Lebanon baada ya mlipuko mkubwa katika mji wake mkuu Beirut.

Shirika la Afya Duniani WHO limewasihi wafadhili kuchangia dola milioni 15 kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya kiafya na kudhibiti kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Uharibifu mkubwa uliofanyika katika bandari ya BeirutPicha: Reuters/M. Azakir

Saudi Arabia imepeleka ndege mbili nchini Lebanon zilizobeba zaidi ya tani 120 za dawa, vifaa vya matibabu, vifaa vya dharura, mahema na chakula kwa ajili ya watu walioathirika na mlipuko mkubwa uliotokea wiki hii. Serikali ya Saudia imesema kikosi maalum kutoka kwenye taasisi ya misaada ya Mfalme Salman kitasimamia usambazaji wa misaada hiyo.

Mjini Paris watu walikusanyika kwenye mkesha maalum usiku wa kuamkia leo kuwakumbuka waliopoteza maisha katika mlipuko mjini Beirut. Walikusanyika nje ya kanisa la Sacre Coeur huku wakiwa wameshikilia bendera kubwa ya Lebanon. Wakati huohuo, Padri wa kanisa kuu la mjini Paris Fadi El Mir aliyeongoza sala kwa ajili ya watu walioathiriwa aliwalaumu wanasiasa kwa matataizo ya nchini humo.

Kwingineko ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inataka ufanyike uchunguzi huru na imesisitiza kwamba mwito wa watu walioathirika juu ya uwajibikaji lazima usikilizwe. Hata hivyo, rais wa Lebanon Michel Aoun ametupilia mbali miito yoyote ya kuwashirikisha wachunguzi kutoka nje ya nchi hiyo.

Rupert Colville, msemaji wa kamishna mkuu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa iongeze juhudi za kuisaidia Lebanon kwa haraka. Amesema Lebanon inakabiliwa na majanga matatu ambayo ni mgogoro wa kiuchumi, COVID-19 na mlipuko uliosababisha vifo na uharibifu mkubwa.

Vyanzo:/AP/RTRE/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW