Watu 43 wauawa kwenye milipuko ya mabomu
13 Novemba 2015Milipuko hiyo imetokea katika mtaa wa shughuli nyingi za biashara wa Burj al-Barajneh, ambako kundi la Hezbollah ambalo wafuasi wake wengi ni wa madhehebu ya Shia, linao umaarufu mkubwa.
Shirika la msalaba mwekundu limesema mbali na watu 43 waliouawa, wengine karibu 240 wamejeruhiwa katika milipuko hiyo, wengi wakiripotiwa kuwa katika hali mahtuti. Mashambulizi hayo yanakumbushia kampeni dhidi ya Hezbollah kati ya mwaka 2013 na 2014 kama ulipizaji kisasi kwa uamuzi wa kundi hilo kuunga mkono kijeshi serikali ya Syria dhidi ya makundi ya waasi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Haya ni mashambulizi makubwa zaidi kuwahi kudaiwa kutekelezwa na kundi la dola la kiislamu nchi Lebanon, na lenye umwagaji mkubwa wa damu tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1975 na 1990.
Hivi leo familia zilijianda kuondoa miiili ya wapendwa wao kutoka hospitalini huku nchi hiyo iitangaza siku ya kitaifa ya maombolezo ambayo imetangazwa na waziri mkuu Tammam Salam.
Shule zimefungwa kwa siku ya leo,huku wanasiasa wa pande zote wakishutumu mashambulizi hayo.
Milipuko hiyo ilisikika karibu na soko lililo karibu na watu masikini la watu wa madhehebu ya Shia huku damu ikitapakaa kwenye sakafu na maduka yaliyo karibu .
Jeshi la nchi hiyo limesema mashambulizi hayo yalitekelezwa na watu wawili wa kujitoa mhanga,na mwili wa mtu wa tatu aliyejitoa mhanga ambaye bomu lake halikulipuka, silaha yake ilikutwa katika eneo la mlipuko wa pili.
Kauli ya Dola la Kiislam ya kutekeleza mashambulizi
Lakini dola la kiislamu limetoa kauli tofauti kwenye taarifa yake kwenye mtandao wakidai kuhusika na mashambulizi hayo.
Taarifa yao imesema na hapa ninanukuu "wanajeshi wetu wa kiislamu walilipua vilipuzi vilivyokuwa vimefungwa kwenye piki piki mjini.Baada ya walioasi kukusanyika katika eneo hilo mmoja wa wanajeshi wetu alilipua kilipuzi katikati yao " mwisho wa kunukuu.
Taarifa hiyo haikuelezea kuhusika kwa Hezbollah katika nchi jirani ya Syria ambayo eneo lake kubwa linadhibitiwa na dola la kiislamu la IS,badala yake limetumia klugha ya mrengo wa kidini yenye kubeza madhehebu ya Shia.
IS ambalo ni kundi la madhehebu ya Sunni huwachukulia watu washia na waislamu wengine wasiokubali tafsiri yake ya dini ya kiislamu, kama waasi wa dini.
Taarifa hiyo haikuweza kuthibitishwa mara moja ,lakini ilifuata utaratibu wa kawaida wa madai ya kuhusika kwa kundi la dola la kiislamu na kusambazwa kwenye mitandao ya makundi ya kigaidi.
Matangazo ya televisheni nchini Lebanon yaliangazia mashambulizi hayo .
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki moon aliyalaani mashambulizi hayo huku akitaka vikosi vya usalama vya Lebanon kutoyaruhusu kuvuruga hali ya utulivu nchini humo.
Mwandishi:Bernard Maranga/AFP/Reuters
Mhariri: Gakuba Daniel