Lebanon yasema mashambulizi ya Israel yameuwa Wasyria 10
18 Agosti 2024Wizara ya afya nchini Lebanon imesema mashambulizi ya anga ya Israel upande wa kusini siku ya Jumamosi yaliua Wasyria 10, huku jeshi la Israel likiripoti kuyashambulia maghala ya silaha ya kundi la wanamgambo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Idadi ya watu waliofariki kutokana na mashambulizi hayo katika eneo la Wadi al-Kafur huko Nabatieh ni kubwa zaidi kutokea kwa siku moja tangu Hezbollah ilipoanza kupambana na jeshi la Israel karibu kila siku katika eneo la mpaka baada ya vita vya Gaza kuzuka Oktoba mwaka jana.
Soma zaidi. Kamanda wa Hezbollah auawa katika shambulizi la anga
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati alimwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy katika wito kwamba kuna "haja ya kuishinikiza Israel kuacha kuishambulia miji na vijiji vilivyopo kusini mwa nchi hiyo."
Wizara ya mambo ya nje ya Syria imeyalaani mashambulizi hayo ya anga, na kuyataja kuwa ni "uhalifu wa wazi dhidi ya mamlaka ya Lebanon na ardhi yake."