1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yaua watu 15 Lebanon

Josephat Charo
25 Septemba 2024

Jeshi la Israel limesema linafanya mashambulizi mengi ya kutokea angani kusini mwa Lebanon na katika bonde la mashariki la Bekaa, baada ya kundi la Hezbollah kufyatua kombora la masafa marefu hadi mji wa Tel Aviv.

Libanon Akbiyeh 2024 | Rettungskräfte untersuchen Trümmer nach israelischem Luftangriff
Picha: Mahmoud Zayyat/AFP/Getty Images

Lebanon imesema watu watatu wameuliwa kufuatia shambulizi la Israel katika kijiji cha Maaysra katika wilaya ya Keserwan kaskazini mwa mji mkuu Beirut.

Shirika la habari la serikali ya Lebanon limeripoti kwamba maroketi mawili yameanguka katika kijiji cha Maaysra, chenye idadi kubwa ya Washia katika eneo la milima la wakristo la Keserwan kiasi kilometa 25 kutoka mji mkuu, Beirut, huku wakithibitisha shambulizi hilo limekilenga kijiji chao na kuharibu nyumba moja pamoja na mgahawa.

Hakuna taarifa za majeruhi zilizotolewa lakini ilikuwa mara ya kwanza kwa eneo hilo kushambuliwa katika makabiliano ya hivi karibuni kati ya jeshi la Israel na kundi la Hezbollah.

Soma pia: Guterres aonya Lebanon kugeuka Gaza nyingine

Kundi la Hezbollah limesema limefyetua kombora la masafa marefu kuyalenga makao makuu ya idara ya ujasusi ya Israel, Mossad, karibu na mji wa Tel Aviv, ikisema mashambulizi dhidi ya kundi hilo la wanamgambo yalipangwa kutokea hapo.

Katika taarifa yake Hezbollah imesema kombora hilo limevurumishwa mwendo wa saa kumi na mbili unusu leo asubuhi kuyalenga makao hayo makuu, yaliyo katika viunga vya Tel Aviv, ambayo yametumiwa kuwaua viongozi wa kundi hilo na kusababisha mlipuko wa vifaa, wakizungumzia mashambulizi ya wiki iliyopita yaliyowaua watu kadhaa nchini Lebanon, akiwamo kamanda wa cheo cha juu.

Papa Francis ataka machafuko yakome

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis, amekosoa hali mbaya ya machafuko inayoendelea kuongezeka katika mgororo wa Lebanon akisema haikubaliki, kufuatia mashambulizi ya mabomu ya Israel kuua mamia ya watu kusini mwa Lebanon.

''Nimehuzunishwa na habari zinazotoka Lebanon, ambako milipuko ya mabomu imesababisha vifo na uharibifu katika siku za hivi karibuni. Nina matumaini jumuiya ya kimataifa itafanya kila juhudi kukomesha ongezeko hili la machafuko ya kutisha. Hali hii haikubaliki. Ninawaombea na niko karibu na watu wa Lebanon, ambao tayari wameteseka sana katika siku za hivi karibuni. Tuwaombee wote wanaoteseka kwa sababu ya vita.''

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa FrancisPicha: Dita Alangkara/AP/dpa/picture alliance

Soma pia: Kijiji cha milimani chashambuliwa kaskazini mwa Beirut

Hii ni mara ya kwanza kwa kundi la Hezbollah kudai kufanya shambulizi la kombora la masafa marefu tangu vita vyake na Israel vilipoanza baada ya kundi la Hamas kufanya shambulizi kubwa nchini Israel mnamo Oktoba 7 mwaka uliopita. Jeshi la Israel limesema hii ni mara ya kwanza kabisa kwa kombora lililofyetuliwa na Hezbollah kuwahi kufika Tel Aviv kabla kuzuiwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa makombora.

Kundi la Hezbollah pia limesema limefanya shambulizi hilo kuonesha mshikamano na watu wa Ukanda wa Gaza na kwa kuilinda nchi ya Lebanon pamoja na watu wake.

Khamenei akosoa mauaji ya makamanda wa Hezbollah

Wakati haya yakiarifiwa, kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei amesema hatua ya Israel kuwaua makanda wa ngazi za juu wa kundi la Hezbollah haitalisambaratisha kundi hilo linaloegemea Iran.

Katika mkutano na maafisa wa jeshi na wanajeshi wastaafu waliopigana katika vita vya Iran na Iraq kati ya mwaka 1980 na 1988, Khamenei amesema muundo na nguvu ya Hezbollah ni zaidi ya kuuliwa kwa makamanda hao wa Hezbollah na mamlaka, uwezo na nguvu yao ni kubwa zaidi na haiwezi kuathiriwa na mauaji hayo.

Khamenei alisema Hezbollah imekuwa ikiulinda ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa mgogoro. "Hadi leo, ushindi umekuwa wa upinzani wa Palestina na Hezbollah," alisema Khamenei. "Ushindi wa mwisho utakuwa kwa vuguvugu la upinzani na Hezbollah."

(afpe, reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW