1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon yawaachilia huru maafisa wanne wa kijeshi.

Munira Mohammad30 Aprili 2009

Mahakama maalum ya Lebanon imeamuru kuachiliwa huru kwa magenerali wanne wa kijeshi wanaounga mkono Syria waliokuwa wanazuiliwa kufuatia mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri.

Rafik Hariri, waziri mkuu wa zamani wa Lebanon mauaji yake yalisababisha kukamatwa kwa maafisa 4 wa kijeshi.Picha: AP


Mjini Beirut milio ya risasi, kusherehekea uamuzi huo ilisikika muda mfupi tu baada mahakama hiyo maalum, iliyo nchini uholanzi kutoa uamuzi wake. Mauaji ya Rafik Hariri mwaka wa 2005, yalisababisha Syria kuondoa majeshi yake nchini Lebanon, baada ya kuwepo nchini humo kwa miaka 29.


Uamuzi huo uliotolewa jana na mahakama maalum yenye makao yake huko The Hague nchini Uholanzi inafunga kurasa, ya Lebanon kuelekeza kidole cha lawama kwa Syria kwa mauaji ya Rafik Hariri.


Saad Hariri, mtoto wa Rafik Hariri akaribisha uamuzi wa mahakama maalum.Picha: AP

Mwaka wa 2005 Hariri ambaye alikuwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon aliuawa na mripuko wa bomu mjini Beirut, pamoja na watu wengine 22. Wanasiasa nchini Lebanon akiwemo mtoto wa Hariri Saad al Hariri walielekeza kidole cha lawama kwa Syria.


Syria ilikana kuhusika na mauaji hayo- ingawa shtuma kutoka kila upande zilifanya Syria kuondoa majeshi yake nchinI Lebanon. Majeshi ya Syria yalikuwa nchini Lebanon kwa miaka 29- kabla ya kuondoka mwaka wa 2005.


Muda mfupi baadaye maafisa wanne wakuu katika jeshi la Lebanon ambao waliiunga mkono Syria, walikamatwa na wamekuwa wanazuiliwa katika jela la Roumieh, Kaskazini mwa Beirut kwa miaka minne- licha ya kuwa hawakufunguliwa mashtaka yeyote.


Mahakama hii maalum jana ikaagiza kuachiliwa huru kwa maafisa hao wanne. Haijabaina iwapo wanne hao watafunguliwa mashtaka baadaye. Mwendeshaji mashtaka Daniel Bellemare, akiwasilisha maoni yake mahakamani alisema kwa sasa hakuna ushahidi wa kutosha wa kuwashtaki washukiwa katika mauaji hayo ya Hariri.


Mjini Beirut, milio ya risasi ilisikika pale wafuasi wa maafisa hawa wanne walipokuwa wakisherehekea uamuzi wa mahakama wa kuwaachilia huru.


Bango lenye picha ya Rais Bashar Assad, wa Syria kushoto na Hassan Nasrallah kiongozi wa Hezbollah.Picha: AP

Uamuzi huu uliotolewa na mahakama maalum yenye makao yake huko The Hague nchini Uholanzi ni pigo kubwa kwa muungano unaopinga ushawishi wa Syria nchini Lebanon- na hasa mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi nchini Lebanon mapema mwezi Juni.


Kundi la Hezbollah na washirika wengine wa Syria watatumia sasa wameweka gei ya juu kupata wingi wa kura bungeni- na uamuzi huu unawapa motisha zaidi.



Saad Hariri-ambaye ni mwanasiasa maarufu nchini Lebabon- aliupokea uamuzi wa mahakama hiyo maalum wa kuwaachilia huru maafisa hao wanne wa kijeshi akisema uamuzi huo haukuwa na upendeleo wala haukuegemea upande wowote wa kisiasa.


Meja Generali Jamil Sayyed mmoja wa maafisa hao walioachiliwa huru- hakuna na mazuri ya kusema kuhusiana na idara ya mahakama ya Lebanon. Alishtumu sheria nchini Lebanon kwa kuwazuilia kwa miaka minne bila ya kuwafungulia mashtaka.



Mwandishi: Munira Muhammad/ Reuters

Mhariri: Abdulrahman