Lehmann amrithi Klinsmann Hertha Berlin
10 Mei 2020Klinsmann alilazimika kujiuzulu kutoka bodi hiyo baada ya kuachia ngazi kama kocha wa mpito wa klabu hiyo ya Bundesliga mnamo mwezi Februari. Aliukosoa uongozi wa timu hiyo katika tangazo lake la kujiuzulu lakini akasema anataraji kubakia katika bodi.
Hertha hata hivyo walisema wamepoteza imani naye na hawakutaka kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani kushika wadhifa wowote katika klabu hiyo.
Lehmann, mwenye umri wa miaka 50, aliwahi kuichezea Schalke, AC Milan, Borussia Dortmund, Arsenal na VfB Stuttgart. Katika siku za hivi karibuni alikuwa kocha msaidizi wa klabu ya Augsburg inayocheza katika ligi kuu.
Kocha wa Hertha kwa sasa ni Bruno Labbadia, ambaye ataiongoza timu hiyo kwa mechi yake ya kwanza watakapokabana koo na Hoffenheim ugenini Jumamosi, huku Bundesliga ikirejea tena baada ya kusimamishwa kwa muda wa miezi miwili kutokana na janga la virusi vya corona.
(dpa)