1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leicester ni mabingwa wa soka Uingereza

Admin.WagnerD3 Mei 2016

Maelfu wamesheherekea na mamilioni duniani kupigwa na mshangao wakati timu ya Leicester ambayo haikufikiriwa kunyakuwa ubingwa ilipoutwaa ubingwa wa soka wa Uingereza na kuweka historia katika kabumbu la Uingereza.

Picha: picture-alliance/dpa/T. Keeton

Timu iliokuwa ikishika nafasi yapili katika Ligi Kuu ya Uingereza Tottenham Hottspurs ilitoka sare ya mabao 2-2 na Chelsea Jumatatu (02.05.2016) usiku kwa timu hiyo ambayo mwaka jana ilikuwa nusura ishuke daraja kuweza kuukwaa ubingwa huo adimu kabisa kwake baada ya kun'gara dhidi ya timu nyengine nguli za Uingereza .

Ushindi wa michezo 22 kati ya 36 wa Leicester hadi sasa katika msimu huu wa ligi ambao bado unaendelea na ikiwa imepoteza michezo mitatu tu inamaanisha kwamba imekuwa mabingwa ikiwa bado imebakisha michezo miwili huku timu za Arsenal, Manchester City,Manchester United na Liverpool zikifuatia.

Baada ya kuepuka kushushwa daraja mwaka jana na nafasi ya kutwaa ubingwa ikitabiriwa kuwa moja kati ya 5,000 mwanzoni mwa ligi kuu hiyo ya Uingereza timu hiyo chini ya kocha Claudio Ranieri hivi sasa imeleta mshutuko ambao wengi hawakuwahi kushuhudia katika michezo.

Timu hiyo ya daraja la wastani ya eneo la Midlands ni mabingwa wa kwanza wa Uingereza tokea timu ya Nottingham Forest chini ya kocha Brian Clough kufanya hivyo mwaka 1978 na kuiibuka kwao katika mpambano wa ligi ya soka unaoangaliwa mno duniani umewapatia mashabiki duniani kote.

Kiwewe cha mashabiki

Mashabiki wa Leicester City (02.05.2016)Picha: Reuters/E. Keogh

Mashabiki waliokuwa wakicheza huku wakipeperusha bendera rangi ya buluu na nyeupe walimiminika majiani huko Leicester wakati video katika mtandao wa Twitter zikionyesha timu hyo ikisheherekea kwa kiwewe kufuatia ushindi wao huo.

Shabiki mmoja amesikika akisema "Kuitaja Leicester na ligi ya Mabingwa wa Ulaya katika sentensi moja ni jambo ambalo mtu hawezi kuamini kaka !"

Wakati Ligi ya Uingereza likiwa ni tukio kubwa la michezo duniani likivutia mabilioni ya paundi za Uingereza katika mikataba ya kuonyeshwa kwenye televisheni ushindi huo wa Leicester umekuwa ukifuatiliwa duniani kote.


Mara ya mwisho timu hiyo ilifanya vizuri katika michuano ya ligi kuu ya Uingereza ilikuwa ni mwaka1929 wakati iliposhika nafasi ya pili na kombe la mwisho lilikuwa lile "Kombe la Ligi " hapo mwaka 2000.

Fahari ya kocha

Timu hiyo sasa inasubiri kwa hamu tafirija nyengine wakati watakapobeba kombe hilo la ubigwa katika uwanja wao wa Power King kufuatia mchezo wao Jumamosi dhidi ya Everton.

Kocha wa timu ya Leicester City Claudio Ranieri.Picha: Getty Images/M. Regan

Ranieri ambaye iliripotiwa kwamba alikuwa akirudi Uingereza kutokea Italia ambako alikwenda kumtembelea mama yake mwenye umri wa miaka 96 wakati matokeo hayo yalipokuja hapo Jumatatu amesema kamwe hakutegemea kushinda taji hilo wakati alipoajiriwa mwaka jana.

Mtaliana huyo mwenye umri wa miaka 64 amesema anaona fahari katu hakutegemea na kwamba yeye ni mtu mwenye kuangalia uhalisia.

Ranieri katu hakuwahi kushinda kombe la ligi hapo kabla na alitimuliwa na Chelsea hapo mwaka 2004 lakini mayowe "Kuna Ranieri mmoja tu" yalihanikiza kwenye uwanja wao wakati kipenga cha mwisho katika pambano hilo la Jumatatu kikikaribia kupulizwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW