1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni siku ya mwisho kwa majeshi ya Uingereza kuwepo Iraq

Kabogo Grace Patricia31 Julai 2009

Mkataba uliosainiwa na nchi hizo mbili, unaitaka Uingereza kuondoa majeshi yake yote ifikapo Julai 31, 2009.

Mwanajeshi wa Uingereza akipunga mkono wakati akifanya doria katika gari ya deraya mjini Basra.Picha: AP


Leo ni siku ya mwisho kwa majeshi ya Uingereza kuondoka rasmi nchini Iraq, baada ya kuwepo nchini humo kwa muda wa miaka 6 kufuatia uvamizi ulioongozwa na Marekani na kumtoa madarakani, Saddam Hussein. Chini ya mkataba kati ya Iraq na Uingereza uliosainiwa mwaka uliopita, majeshi ya mwisho ya Uingereza yanatakiwa kuondoka nchini Iraq ifikapo Julai 31, mwaka huu.

Nchi hizo mbili zilitiliana saini kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai, mwaka huu majeshi yote ya Uingereza yawe yameondoka nchini Iraq, mara baada ya majeshi hayo kumaliza kazi yake, ambapo katika miezi ya hivi karibuni majeshi hayo yalikuwa yakitoa mafunzo kwa jeshi la Iraq.

Msemaji wa Ubalozi wa Uingereza nchini Iraq, amesema mkataba mpya kuhusu wanajeshi wa maji wanaotoa mafunzo kurejea nchini Iraq umeidhinishwa na baraza la mawaziri la Iraq na Uingereza, ikiwa ni sehemu ya kikosi cha majeshi ya NATO nchini humo na kutoa nafasi kwa maafisa wa jeshi la Iraq kuhudhuria mafunzo nchini Uingereza.

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair aliungana na Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush wa Marekani, kuivamia Iraq mwaka wa 2003, na kufanikiwa kumuondoa madarakani Saddam Hussein kwa madai kuwa alikuwa akitengeneza silaha za maangamizi. Tangu wakati mwaka huo wa 2003, wanajeshi 179 wa Uingereza wameuawa nchini Iraq. Wengi wa wanajeshi wa Uingereza walikuwa wamewaka kambi katika mji wa Basra uliopo kusini mwa Iraq, mji unaokaliwa na Washia. Uingereza ni nchi ya pili kuwa na idadi kubwa ya wanajeshi baada ya Marekani, ambapo ilikuwa na wanajeshi 46,000. Hata hivyo, Uingereza imehamishia majeshi yake katika ngome ya Taliban nchini Afghanistan.

Kuondoka kwa wanajeshi wa Uingereza nchini Iraq kunafanyika miaka 50 baada ya Uingereza ya zamani kuondoka nchini Iraq Mei, mwaka 1965, wakati wanajeshi wa mwisho walipoondoka Habbaniyah karibu na mji wa Fallujah. Pia majeshi hayo yanaondoka mwezi mmoja tangu majeshi ya Marekani yajiondoe katika miji ya Iraq ikiwa ni katika mkataba baina ya nchi hizo mbili kuwa majeshi yote ya Marekani yataondoka Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka 2011.

Aidha, majeshi ya Uingereza yanaondoka nchini Iraq siku moja baada ya kuanza kwa uchunguzi kuhusu nchi hiyo ilivyoshiriki katika vita vya Iraq. Tume hiyo itawahoji viongozi kadhaa wa nchi hiyo, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani, Tony Blair na itakuwa na huru kukosoa maamuzi yaliyofanywa na serikali. Mwenyekiti wa tume hiyo, Sir John Chilcot amesisitiza kuwa tume yake itazuru Iraq kwa mazungumzo na maafisa wa nchi hiyo na maafisa wa Marekani na nchi nyingine zilizoshiriki katika vita hivyo. Hata hivyo, Chilcot amesema Blair ameahidi kutoa ushirikiano kwa tume hiyo. Mwezi uliopita, mrithi wa Blair, Gordon Brown, alitangaza kuanza kwa uchunguzi huo, akitekeleza ahadi yake aliyotoa ya kufanyika kwa uchunguzi, pindi majeshi ya Uingereza yatakapoondoka nchini Iraq.

Uamuzi wa Uingereza kuungana na Marekani kuivamia Iraq, ulipingwa na wananchi wengi wa Uingereza akiwemo Waziri Robin Cook.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: M. Abdul-Rahman



Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW