1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eid Mubarak kwa waislamu wote

10 Aprili 2024

Waislamu takribani kote duniani wanasherehekea sikukuu ya Eid-ul-Fitr baada ya kuukamilisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, huku baadhi ya mataifa ya Kiislamu yakikabiliwa na hali ngumu ya vita na njaa.

Bangladesch Islam l Eid-ul-Fitr, Fest des Fastenbrechens in Dhaka
Picha: Stringer/AA/picture alliance

Tangazo lililotolewa jioni ya Jumanne (Aprili 9) na ofisi za kidini kote Afrika Mashariki lilikwenda sambamba na lile lililotolewa nchini Saudi Arabia, iliko misikiti miwili mitukufu kabisa kwa Waislamu, kwamba siku ya Jumatano ingelikuwa Eid Mosi.

Qatar, Oman, Muungano wa Falme za Kiarabu na Iran nazo pia ziliadhimisha sikukuu hiyo kwa siku moja, hali ya nadra sana kwa sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu kufunguwa saumu zao kwa pamoja.

Soma zaidi: Waislamu Uganda waadhimisha Eid-ul-Fitr wakilaani vita vya Sudan

Mataifa mengi yalitangaza siku nne za mapumziko kusherehekea kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, nguzo ya nne katika nguzo tano za Uislamu, ambapo waumini walikuwa wakijizuwia kula, kunywa na mambo yote yanayokatazwa kuanzia asubuhi hadi jioni. 

Sala za Eid ziliswaliwa kwenye misikiti mikubwa na maeneo mbalimbali ya wazi wakati asubuhi.

Eid katikati ya mauaji Ukanda wa Gaza

Kwa ujumla sikukuu ya mwaka huu ilitandwa na kile kilichokuwa kinaendelea kwenye Ukanda wa Gaza, ambako mashambulizi ya Israel yameshauwa zaidi ya watu 33,000, zaidi ya nusu wakiwa wanawake na watoto kwa kipindi cha miezi sita mfululizo. 

Hali ya Ukanda wa Gaza baada ya miezi sita ya mashambulizi ya Israel.Picha: Tedros Adhanom Ghebreyesus/Handout/REUTERS

Juhudi za wapatanishi kupata makubaliano ya kusitisha mapigano kabla ya Ramadhani yalikwama na kulikuwa na wasiwasi kwamba Israel ingeliendelea na mashambulizi ya ardhini kwenye eneo la kusini la Rafah, ambako mamilioni ya Wapalestina wamekimbilia kusaka hifadhi.

Soma zaidi: Israel yaidhinisha operesheni ya kijeshi Rafah

Mazungumzo ya kutafuta suluhu yalikuwa yanaendelea mjini Cairo, Misri, ingawa hakukuwa na mafanikio yoyote. 

Misamaha kwa wafungwa  

Nchini Bahrain, mamlaka za nchi hiyo ziliwaachilia huru watu 1,584 waliokuwa wakikabiliwa na mashitaka ya uhalifu na kufanya ghasia, ikiwa sehemu ya kuadhimisha sikukuu ya Eid-ul-Fitr, ambayo mwaka huu ilisadifiana na maadhimisho ya miaka 25 tangu Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa kutawala.

Walinzi wa mazingira walioachiwa huru nchini Iran.Picha: sharghdaily

Msamaha pia umetangazwa nchini Iran kwa walinzi wanne wa mazingira, ambao wametumikia kifungo cha miaka kadhaa jela.

Soma zaidi: Marekani yajitayarisha na kitisho cha shambulizi la Iran

Wanamazingira hao, Niloufar Bayani, Houman Jokar na mkewe Sepideh Kashani, pamoja na mwanabailojia Taher Ghadirian, waliachiwa jioni ya jana. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) lilisema lilikuwa limengojea kwa miaka sita uamuzi kama huo kufikiwa.

Ulinzi waimarishwa

Nchini Pakistan, mamlaka zilituma askari na vikosi vya wanamgambo zaidi ya 100,000 kwenye maeneo ya misikiti na masoko kote nchini humo kulinda usalama wakati huu wa sherehe za Eid.

Ulinzi waimarishwa kwa sikukuu ya Eid-ul-Fitr nchini Pakistan.Picha: Faruq Azam/DW

Ingawa mashambulizi kwenye siku za sikukuu huwa ni ya nadra nchini humo, Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema ilikuwa imepokea taarifa za kijasusi kuwa makundi ya wanamgambo yanangeliweza kutumia sherehe hizo kuwashambulia raia, majengo ya serikali na jeshi pamoja na maeneo yanayokaliwa na polisi.

Soma zaidi: Mahakama ya Pakistan yakubali rufaa ya Khan ya hatia ya ufisadi

Hali kama hiyo inashuhudiwa pia kwenye nchi jirani ya Afghanistan, ambako utawala wa Taliban ulisema uko kwenye hali ya hadhari katika sikukuu hizi za Eid-ul-Fitr.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Abdul Mateen Qani alisema vikosi vya walinda usalama vilitumwa kwenye maeneo yote ya mikusanyiko ya watu, ikiwemo misikiti.

Rais wa Ujerumani atuma salamu

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani.Picha: Petros Karadjias/AP Photo/picture alliance

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumai alitowa salamu zake za Eid kwa Waislamu akiwatakia mwisho mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

"Kufunga na kufunguwa funga ya Ramadhani ni sehemu ya maisha ya Ujerumani yenye imani za watu mbalimbali. Ukweli kwamba leo, mwishoni mwa mwezi wa mfungo, jamii za Waislamu kote nchini zinawaalika wanaadamu wenzao wa imani nyengine ni ishara muhimu ya uvumilivu na heshima na nia ya kuishi pamoja na kubadilishana mawazo." Alisema kiongozi huyo.