1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni Sikuu Kuu ya Idd el Hajj kwa Waislamu

19 Desemba 2007

MECCA

Waislamu leo wanaungana na wenzao duniani kote kusheherekea Siku Kuu ya Id el Hajj kufuatia kumalizika kwa ibada ya Hijja mjini Mecca Saudi Arabia.

Hapo jana jioni mamilioni ya mahujaji wa Kiislam walielekea Muzdalifa baada ya kutumia kutwa nzima kwenye Mlima Arafa mashariki mwa Mecca ikiwa ni kilele cha ibada hiyo ya Hija inayofanyika kila mwaka.

Wakiwa Muzdalifa katika hatua nyengine ya ibada hiyo Waislamu watakusanya vijiwe vya kupiga nguzo zilizomithillishwa na shetani kwa siku tatu kumlaani shetani.

Wakiwa kwenye Mlima Arafa hapo jana Waislamu waliomba dua na msamaha kwa Mwenyeenzi Mungu na ustawi wa Waislamu duniani kote.

Waislamu wanatumia siku kuu ya leo kwa kuchinja wanyama aidha kondoo ama mbuzi kuadhimisha kumalizika kwa hija kwa kuigiza tendo la Nabii Ibrahim aliekuwa tayari kumtolea muhanga mwanawe wa kiume Ismail kwa ajili ya Mwenyeenzimungu.

Serikali ya Saudi Arabia imesema watu milioni 1.6 wameingia nchini humo kutoka nje kwa ajili ya ibada hiyo ya Hijja ambayo kwa jumla watu milioni sita walikuwa wakitegemewa kuhiji.

Hija ni mojawapo ya nguzo tano kuu za Uislamu ambapo Muislamu anatakiwa kuitimiza angalau mara moja katika uhai wake iwapo ana uwezo na afya.