1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bonucci kuishtaki Juventus kwa kumlazimisha kuondoka klabuni

14 Septemba 2023

Leonardo Bonucci aliyejiunga na klabu ya Union Berlin inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga amejibu madai yaliyotolewa na Juventus na kwamba aliwahi kupewa "fursa ya kuendelea na kuongeza mkataba."

Italien Fußball Serie A |  Udinese Calcio - Juventus FC
Leonardo Bonucci alipokuwa Juventus.Picha: Ettore Griffoni/LiveMedia/ipa/picture alliance

Beki wa klabu ya Union Berlin inayoshiriki Ligi Kuu ya Kandanda hapa Ujerumani Bundesliga Leonardo Bonucci, amejibu madai mbalimbali yaliyotolewa kuhusu kuondoka kwake katika klabu ya Juventus, akidai kwamba aliwahi kupewa "fursa ya kuendelea na kuongeza mkataba."

Soma zaidi: Rubiales atafikishwa mahakamani Ijumaa

Bonucci mwenye umri wa miaka 36 aliondolewa katika kikosi cha Massimiliano Allegri cha Juventus katika msimu huu wa joto baada ya kuachwa mjini Turin wakati wa ziara ya mechi za kujiandaa na msimu mpya wa klabu hiyo nchini Marekani.

Leonardo Bonucci amejiunga na FC Union Berlin ya UjerumaniPicha: Matthias Koch/IMAGO

Bonucci alilazimishwa kuondoka Juventus kabla ya hatimaye kujiunga na Union Berlin katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili ambapo amesaini mkataba wa miaka mmoja huku kukiwepo nafasi ya kuongeza mwaka wa pili zaidi.

Akizungumza na shirika la habari za la Sport Mediaset, Bonucci amepinga madai yaliyotolewa na Juventus katika kipindi cha miezi michache iliyopita.

Soma zaidi: Jorge Vilda afutwa kazi kama kocha wa timu ya wanawake ya Uhispania

Bonucci amesema “Nimesoma na kusikia mambo mengi ambayo si ya kweli, ningependa kuanzia mbali. Kuanzia tarehe hiyo iliyotajwa mara kadhaa na Juventus na kocha, waliposema kwamba wamenifahamisha hali ilivyokuwa msimu huu tayari Oktoba mwaka jana''.

"Haiwezi kuwa kweli, Oktoba mwaka jana kwa kweli nilipewa fursa ya kuendelea na Juventus kwa kuongezewa mkataba."

Beki huyo mkongwe ambaye ameichezea klabu ya mjini Turin zaidi ya michezo 500 kwa kipindi cha miaka 12 ameelezea jinsi alivyodhalilishwa na klabu hiyo katika kipindi hiki cha majira ya joto kwa kulazimishwa kuondoka.

Kocha wa Juventus Massimiliano Allegri alinukuliwa akisema kuwa klabu hiyo ya Italia tayari ilikuwa imemjulisha mchezaji huyo tangu mwezi Februari kwamba itabidi ajitafutie nyumba mpya ikiwa anataka kuongeza muda wake wa kuchezea Juventus.

Kocha wa Juventus Massimiliano Allegri anasema alimshauri Bonucci kustaafu soka baada ya kucheza kwa miaka mingi.Picha: AP

Soma zaidi: FIFA yamsimamisha rais wa shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales

Katika mahojiano hayo, meneja huyo mwenye umri wa miaka 56 alipendekeza kwamba baada ya beki huyo kucheza zaidi ya mechi 500 ni wakati sasa wa kustaafu, japo maneno hayo ya Allegri yamepingwa vikali na Bonucci.

Bonucci anasema "Sikuwa na mazungumzo na klabu wakati huo, lakini nilianza kuhisi kitu niliposoma kwenye magazeti kwamba sitakuwa tena sehemu ya mipango ya kikosi cha Juventus."

Bonucci ameamua kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Juventus, akitarajia kuishtaki klabu yake ya zamani baada ya kuvunja makubaliano ya pamoja akiwa ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW