1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen kileleni mwa Bundesliga

2 Oktoba 2023

Bayer Leverkusen imetulia kileleni mwa jedwali la ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga, wakati Bayern Munich ikiambulia sare ya 2-2 dhidi ya RB Leipzig.

Bayer 04 Leverkusen vs RB Leipzig
Leverkusen washerehekea baoPicha: Marius Becker/dpa/picture alliance

Mbali na haya kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania itawakilishwa na timu mbili katika hatua ya makundi.

Leverkusen iliicharaza bila huruma timu ya mkiani kwenye jedwali la Bundesliga Mainz 05 mabao  3-0 nyumbani, huku Bayern ikishindwa kuifunga RB Leipzig katika mechi ya nne mfululizo. Bayern ililazimisha sare ya 2-2 baada ya kulazwa mabao mawili bila jibu ili kuepuka kichapo cha tatu mfululizo kutoka kwa mabingwa wa Kombe la Ujerumani DFB.

 Soma pia: Leverkusen moto wa kuotea mbali Bundesliga

Lois Openda alipachika wavuni bao la ufunguzi kwa Leipzig dakika ya 20 huku Castello Lukeba akiongeza la pili dakika sita baadaye. Lakini Harry Kane aliwarudisha mchezoni Bavarians kupitia mkwaju wa penalti dakika ya 57 na Leroy Sané akisawazisha katika 70.

Kocha wa Bayern Thomas Tuchel akiwa uwanjaniPicha: Hendrik Schmidt/dpa/picture alliance

Bayern imeshuka hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 14, nyuma ya VfB Stuttgart inayoshika nafasi ya pili pointi moja nyuma ya vinara Bayer Leverkusen walio na jumla ya pointi 16.

Kocha wa Bayern Munich Thomas Tuchel, alikuwa na haya yakusema "Tulionyesha kiwango bora zaidi, tulidhihirisha nguvu na hali nzuri kimchezo. Kwanza kabisa, ulikuwa mchezo mgumu sana katika kipindi cha pili, kama pambano la wazi la ndondi ambalo tunapambana kwa mtoano. Lakini walikuwa vizuri. Tulicheza vizuri na tulistahili kusawazisha."

Union Berlin, ambayo itakuwa inacheza mechi yake ya kwanza ya nyumbani katika ligi ya mabingwa Ulaya hapo kesho Jumanne, itaingia katika mechi hiyo ikiwa imefungwa mechi ya nne mfululizo katika ligi ya Bundesliga, baada ya kulazwa moja mtungi na timu iliyopanda daraja msimu huu Heidenheim.

Stuttgart waliendelea na matokeo mazuri kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya FC Cologne, baada ya mshambuliaji Deniz Undav, akitokea benchi na kucheka na wavu mara mbili.

Soma pia: Ujerumani inaweza kufanya vyema EURO 2024

Darmstadt nayo ilishinda mechi yao ya kwanza ya Bundesliga tangu ilipopanda daraja kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya Werder Bremen jana Jumapili.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW