Leverkusen kukosa huduma za Chicharito
19 Februari 2016Mchezaji huyo raia wa Mexico amekuwa moto wa kuotea mbali tangu alipojiunga na klabu hiyo msimu huu akitokea Manchester United, huku akifunga mabao 13 katika ligi na kufunga jumla ya mabao 22 kwenye michuano 26 katika mashindano yote kufikia sasa.
Lakini maumivu ya musuli aliyopata katika mchuano wa robo fainali wa Kombe la Shirikisho la Ujerumani waliopoteza dhidi ya Werder Bremen wiki iliyopita yamemuweka Chicharito mwenye umri wa miaka 27 nje ya uwanja katika wakati ambapo Leverkusen ilikuwa ikipata matokeo mazuri.
Leverkusen ambao wako nyuma ya Dortmund na pengo la pointi 13, hawajashinda mchuano wowote kati ya nane ya nyumbani dhidi ya klabu hiyo ya bonde la Ruhr.
Dortmund wana mfungaji bora kwa jina Pierre-Emerick Aubameyang ambapo Mgabon huyo amefunga mara 20 katika ligi kufikia sasa.
Dortmund ambao wameshinda mechi zao tatu kati ya nne tangu kipindi cha mapumziko ya kipupwe, wamejiimarisha katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi. Katika michuano mingine ya kesho, Schalke v VfB Stuttgart (1630), Hanover 96 v Augsburg (1630)
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Gakuba Daniel