1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen waongeza mwanya baina yao na Bayern

4 Machi 2024

Matumaini ya mashabiki wa kandanda Ujerumani ya kuwa na bingwa mpya msimu huu yameongezeka baada ya Bayern kulishinda taji mara 11 mfululizo.

1. FC Cologne - Bayer Leverkusen
Jeremie Frimpong wa Leverkusen akisherehekea bao la kwanza dhidi ya FC ColognePicha: Rolf Vennenbernd/dpa/picture alliance

Bayer Leverkusen ambayo haijawahi kulishinda taji la Bundesliga katika historia yao imefungua mwanya wa pointi kumi baina yao na timu iliyo nafasi ya pili Bayern Munich.

Leverkusen walifikia hatua hiyo baada ya kuilaza FC Cologne nyumbani kwao Jumapili 2-0 baada ya Bayern kulazimishwa sare ya 2-2 na Freiburg Ijumaa.

Kocha wa Leverkusen Xabi Alonso lakini hataki kuanza sherehe za ubingwa na mapema kwani bado kumesalia mechi 10 msimu kufikia mwisho na haya ndiyo aliyokuwa nayo baada ya mechi dhidi ya Cologne.

"Haikuwa rahisi kuwafunga hata waliposalia 10 uwanjani, wameonyesha dhamira hata walipokuwa 10. Tulichostahili kufanya ni kuudhibiti mchezo na kusubiri wakati kwa kuwa hatukuwa na nafasi nyingi na haikuwa rahisi hasa kutokana na uwanja ambao ulikuwa na mabonde. Kwa ujumla, hatukufanya la kustaajabisha ila zilikuwa pointi tatu muhimu," alisema Alonso.

Kocha Xabi Alonso akiwa na wachezaji wake Florian Wirtz na Jonathan Tah baada ya mechi na ColognePicha: Rolf Vennenbernd/dpa/picture alliance

Leverkusen kufikia sasa wameweka rekodi Ujerumani kwani hawajafungwa katika mechi 34 katika mashindano yote ila kiungo wao muhimu Granit Xhaka anasema kwa sasa wao kama wachezaji hata fikra zao hazipo kwenye ubingwa.

"Amini usiamini, hatulitazami jedwali, hatutazami aliye nyuma yetu, tunajitazama wenyewe. Tunajua tunastahili kufanya kazi yetu kwanza na tunaifanya. Ila hakuna mchezaji anayelizungumzia taji," alisema Xhaka.

Vyanzo: DPA/AP/Reuters