1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen washinda taji la kwanza la Bundesliga

15 Aprili 2024

Bayer Leverkusen wameshinda taji la ligi kuu ya kandanda Ujerumani - Bundesliga kwa mara ya kwanza katika historia yao ya miaka 120.

Mashabiki wa Leverkusen wakisherehekea ubingwa wa Bundesliga uwanjani Bay Arena
Mashabiki walimwagika katikati mwa uwanja baada ya mechi kukamilika na kusherehekea ubingwa wao wa kwanzaPicha: Amós Fernando/DW

Bayer Leverkusen wameshinda taji la ligi kuu ya kandanda Ujerumani - Bundesliga kwa mara ya kwanza katika historia yao ya miaka 120. Leverkusen iliifunga Werder Bremen mabao matano kwa sifuri Jumapili jioni na kuweka kikomo kwa utawala wa Bayern Munich wa miaka 11 mfululizo wa ligi kuu.

Soma pia: Tuchel kuisusa mechi inayoweza kuipa taji la Bundesliga Leverkusen

Vijana hao wa kocha Xabi Alonso walifahamu kuwa ushindi ungewapa taji zikiwa zimesalia mechi tano msimu kukamilika, na walidhihirisha umahiri wao uwanjani. Florian Wirtz alifunga hartrick na mabao ya Victor Boniface na Granit Xhaka yakarefusha muendelezo wao wa kutopoteza mechi yoyote kati ya 43 walizocheza katika mashindano yote.

Leverkusen walikuwa wamemaliza kama makamu bingwa mara tano katika historia yao na sasa wameiweka hai ndoto yao ya kubeba mataji matatu katika msimu mmoja. Wako katika robo fainali ya Ligi ya Europa na pia watacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Ujerumani - DFB Pokal.

Wana pointi 79 kwa sasa, ikiwa ndio idadi kubwa zaidi ya pointi katika historia ya Bundesliga baada ya mechi 29 na wanaongoza kileleni na pengo la pointi 16 dhidi ya nambari mbili Bayern Munich na Stuttgart katika nafasi ya tatu. Kocha Alonso amesema anatumai ubingwa huo ni kitu kizuri kwa kandanda la Ujerumani kuonyesha kuwa yeyote anaweza kubeba taji na sio Bayern Munich pekee.