1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen yakaribia kuvunja rekodi yaichapa West Ham 2-0

Sylvia Mwehozi
12 Aprili 2024

Vinara wa Bundesliga klabu ya Leverkusen ambao hadi sasa hawajapoteza mchezo, imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya West Ham katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa uwanja wa nyumbani wa BayArena.

Ligi ya Ulaya Bayer Leverkusen Vs West Ham United
Jonas Hofmann akishangilia baada ya kuifungia Leverkusen bao la kwanza dhidi ya West HamPicha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Mabao ya Leverkusen yamepachikwa kimiani na wachezaji Jonas Hofmann na Victor Boniface. Leverkusen ambao ni wawakilishi pekee wa Ujerumani katika michuano hiyo ya ligi ya Ulaya, walitawala mchezo huo lakini walishindwa kupenya lango la West Ham. Zikiwa zimebaki dakika 14 tu mchezo kumalizika, kocha Xabi Alonso, aliwaingiza kutoka benchi Hofman na Boniface na uamuzi wake huo hatimaye ulizaa matunda baada ya kupata bao la kwanza mnamo dakika ya 83 lililofungwa na Hofman.

Mohammed Kudus(katikati) akiwa amebanwa na wachezaji wa LeverkusenPicha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Leverkusen yatinga fainali Kombe la Shirikisho - DFB PokalBoniface alifunga ubao wa matokeo dakika za lala salama, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Hofmann na kuongeza bao la pili na la ushindi. Ushindi huo unaendeleza kicheko kwa Leverkusen, ambao wana pointi 16 mbele ya Bayern Munich na wanaweza kushinda taji lao la kwanza la Bundesliga kwa kuwafunga Werder Bremen nyumbani siku ya Jumapili.

West Ham, ambao walipambana vikali wakiwa na uwezo mdogo wa kumiliki mpira watahitaji kuwa timu ya kwanza kukishinda kikosi cha Alonso msimu huu ili kusonga hatua ya nusu fainali. West Ham watawakosa wachezaji wake wawili kwenye mechi ya marudiano Emerson na Lucas Paqueta walio na kadi za njano.Leverkusen waazimia kunyanyua mataji matatu msimu huu

Mechi nyingine zilizopigwa usiku wa leo ni Atalanta Bergamo na Liverpool. Klabu hiyo inayoshiriki ligi ya Serie A ya Italia imewashangaza wenyeji Liverpool baada ya kuwatandika bao 3-0 katika pigo jingine kubwa kwa kikosi cha Jürgen Klopp.

Wachezaji wa Atalanta Bergamo Picha: Molly Darlington/REUTERS

Gianluca Scamacca amefunga mabao mawili dakika ya 38 na 61, huku Mario Pasalic akihitimisha ushindi kwa bao la tatu dakika ya 83 na kuwaweka vijana wa Kiiitaliano katika nafasi nzuri ya kutinga nusu fainali katika mkondo wa mechi ya pili itakayochezwa nyumbani wiki ijayo.

Liverpool imepokea kichapo hicho ikiwa bado na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 2-2 na Manchester United siku ya Jumapili na kupoteza uongozi wa ligi kuu ya England mbele ya Arsenal.

Mabingwa wa Ureno Benfica wamepata ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Marseille kupitia mabao ya Rafa Silva na fowadi wa Argentina Angel Di Maria.

Roma wamewaadhibu wenyeji AC Milan kupitia bao la kichwa la Gianluca Mancini akiunganisha kona ya Paulo Dybala dakika ya 17 na kutoka na ushindi wa 1-0. Mechi za marudiano zitachezwa wiki ijayo.