Leverkusen yampa mkataba mpya Henrichs
17 Mei 2017Haya ni kwa mujibu wa klabu hiyo ya ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga.
Henrichs mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na Leverkusen akiwa mdogo na alicheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo Septemba 2015. Ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mechi moja pekeyake na ilikuwa dhidi ya San Marino mwezi Novemba mwaka 2016.
Mkataba wake wa awali ulikuwa unakamilika mwaka 2020 na sasa kulingana na duru, mkataba huu mpya umeshuhudia mchezaji huyo kuongezwa mshahara.
"Ninafuraha sana kwa kuwa nimeweza kuwa mchezaji wa kulipwa na nimeweza pia kuichezea timu ya taifa nikiwa Bayer. Baada ya msimu uliokuwa mgumu, nataka kuisaidia klabu hii irudi katika kile kiwango chake cha mchezo," Henrichs alisema katika taarifa.
Leverkusen wamekuwa na msimu mbovu kulingana na kiwango chao, kwani wanaorodheshwa katika nafasi ya 12 katika Bundesliga, mbele ya mechi yao ya kufunga msimu Jumamosi watakapokwaana na Hertha Berlin ugenini. Huku hayo yakiarifiwa, klabu ya Werder Bremen imesema inatarajia kumsajili kiungo Jerome Gondorf wa klabu iliyoshuka daraja ya Darmstadt. Usajili wa Gondorf utakuwa wa pili kwa Bremen ambayo kwasasa iko katika nafasi za katikati katika jedwali la ligi kuu ya Ujerumani, na hii ni baada ya kumsajili beki wa kushoto wa Sweden Ludwig Augustinsson kutoka Copenhagen ya Denmark.
Bremen hawakutoa taarifa zaidi, walilosema ni kwamba Gondorf amepita uchunguzi wa kiafya na kwamaba atatia saini mkataba hivi karibuni.
Mwandishi: Jacob Safari/DPAE
Mhariri: Sekione Kitojo