Li Qiang akosoa dhamira ya kuitenga China kiuchumi
27 Juni 2023Amesema janga la Uviko-19 huenda halitokuwa mgogoro wa mwisho wa kiafya kwa umma ulimwenguni.
Mkutano wa kilele wa jukwaa la kiuchumi duniani umefunguliwa leo huko Tianjin,China, na waziri mkuu wa nchi hiyo Li Qiang amesema nchi yake itachukuwa hatua za kuimarisha masoko, kuunga mkono maendeleo wakati ikitilia mkazo kasi ya mabadiliko ya kuingia kwenye uchumi wa kijani na kufungua kile alichokiita maeneo ya viwango vya juu vya uchumi wa nchi hiyo kwa ulimwengu wa nje.
Mbele ya wajumbe wa mkutano huo ameukosoa mkakati wa nchi za Magharibi wa kutaka kuitenga China.
"Siku hizi baadhi ya watu katika nchi za Magharibi wanapigia upatu mtazamo wa kile kinachoitwa kujiepusha kuitegemea sana na kujiepusha na China. Naamini kwa kiasi fulani misemo hii miwili ni mitizamo isiyokuwa sahihi'' amesema Bw. Qiang.
Kauli hiyo ya waziri mkuu Li Qiang, ilikuwa inailenga tathmini iliyotolewa na rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von Der Leyen ya kuutaka Umoja wa Ulaya ujiepushe kushirikiana na China kidiplomasia na kiuchumi.
Qiang asema mivutano ya kibiashara inazidi kutanuka
Qiang aligeukia pia mivutano ya kibiashara iliyopo kati ya nchi yake China na Marekani, akisema vizingiti vilivyojificha vilivyowekwa na baadhi ya watu, katika miaka ya hivi karibuni , vinazidi kutanuka na kuusukuma ulimwengu katika hali ya mgawanyiko na hata kwenye makabiliano.
Lakini alisema China inapinga vikali hatua ya kuyatumbukiza masuala ya kiuchumi na biashara katika siasa akisema mawasiliano hasa ndio jambo muhimu kuepusha hali ya kutoelewana kati ya mataifa.
Na kwa upande mwingine China ambayo ni taifa linalofanya shughuli nyingi za uvuvi limeridhia rasmi makubaliano ya kupunguza ruzuku ya serikali kwa sekta hiyo ya uvuvi,makubaliano yaliyopitishwa na nchi wanachama wa shirika la biashara duniani WTO mwaka jana.
Mkuu wa WTO aisifu China kwa uamuzi wake kuhusu shughuli za uvuvi
Mkurugenzi mkuu wa WTO Ngozi Okonjo Eweala, katika taarifa kwa mkutano huo wa jukwaa la kiuchumi wa Tianjin amesema China, kama nchi ambayo inaongoza katika shughuli za uvuvi, ni muhimu sana katika utekelezwaji wa makubaliano hayo na juhudi za pamoja katika kulinda bahari, usalama wa chakula na maisha ya binadamu.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya aina yake ya kimataifa,wanachama 164 wa Shirika la biashara duniani WTO wamekubaliana kushirikiana kuelekea kuondowa kabisa, ruzuku za mabilioni ya dola zinazotajwa kuwa hatari kwa shughuli za uvuvi.
Lakini thuluthi mbili ya wanachama wanapaswa kuyaidhinisha makubaliano hayo kufanikisha utekelezaji wake na baadhi ya vipengele vya makubaliano hayo havijakamilishwa.
Tovuti ya WTO inaonesha ni nchi 11 tu mpaka sasa zilizoupitisha rasmi.