1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liberia kupatiwa dawa ya majaribio ya Ebola

12 Agosti 2014

Liberia imetangaza kuwa hivi karibuni itapokea dozi za dawa za majaribio ya kutibu ugonjwa wa Ebola kutoka Marekani, ambazo itazitumia kwa madaktari wawili walioambukizwa virusi hivyo.

Ebola Krankenhaus Liberia
Picha: Reuters/Samaritan's Purse

Serikali ya Marekani ilithibitisha kuwa iliwaunganisha maafisa wa Liberia na kampuni inayotengeneza dawa hiyo iitwayo ZMapp. Katika taarifa yake, kampuni hiyo ya Mapp Biopharmarceutical yenye makao yake jimboni California, ilisema kuwa katika kujibu maombi kutoka kwa taifa la Afrika magharibi ambalo halikutajwa, ilikuwa imeishiwa na ugavi wa dawa hiyo.

Habari hizo zinakuja huku ghadhabu zikiongezeka kuhusiana na ukweli kwamba watu pekee waliopatiwa dawa hiyo ya majaribio ni kutoka mataifa ya magharibi - Wamarekani wawili na Mhispania ambao wote walirudishwa nyumbani kwao kutoka Liberia.

Wauguzi wa Liberia wakiondoa mwili wa muhanga wa Ebola nyumbani katika viunga vya mji wa Monrovia.Picha: picture-alliance/dpa

Idadi ya vifo yaongezeka

Jumatatu jioni, shirika la afya duniani WHO, lilisema watu 1,013 wamekufa kutokana na ugonjwa wa Ebola katika mataifa ya Afrika ya Magharibi, huku serikali zikibainisha washukiwa wa ugonjwa huo 1,848. Idadi hiyo ya WHO inahusisha takwimu za kaunzia Agosti 7 hadi 9, ambapo watu 52 zaidi walikufa kutoka na ugonjwa huo, na 69 zaidi waliambukizwa.

Lakini mfanyakazi wa shirika la misaada la Madktari wasio na mipaka MSF nchini Liberia, Cokie Van Der Velde anasema hali ni mbaya kuliko inavyodhaniwa."Kiukweli idadi ya waliokufa na walioathirika haionyeshi hali halisi," alisema Van Der velde na kuongeza kuwa kuna vifo vijijini na nchini kote ambavyo havirekodiwi kwa sababu ukusanyaji wa data siyo mzuri kama unavyopasa kuwa.

"Nadhani nchini Liberia ugonjwa huo uko katika kaunti sita na unazidi kusambaa. Na unaweza kuenea katika kanda nzima ya Afrika Magharibi, hivyo ni hali ngumu."

Bado hakuna tiba ya uhakika

Hakuna chanjo wala tiba ya Ebola hadi sasa, lakini kuna dawa kadhaa za majaribio mbali na ZMapp. Tiba hiyo bado ni mpya sana kiasi kwamba haijafanyiwa majaribio ya usalama au ufanisi kwa binaadamu. Na kampuni inayoitengeneza imesema itachukuwa miezi kadhaa kutengeneza wingi wa kutosha.

Haikuwa bayana ni kiasi gani cha dawa hiyo kitapelekwa nchini Liberia. Wizara ya afya ya Marekani ilisema katika taarifa kuwa serikali ya Marekani ilisaidia kuiunganisha serikali ya Liberia na mtengenezaji wa dawa hiyo, na kuongeza kuwa kwa sababu inasafirishwa kutumiwa nje ya Marekani, taratibu zote za usafirishaji wa nje zilipaswa kufuatwa.

Muuguzi akijipuliza dawa za kuzuwia maamukizi ya Ebola.Picha: picture-alliance/dpa

Taarifa ya Liberia iliyowekwa kwenye tovuti ya ofisi ya rais, ilisema nchi hiyo ilikuwa inapokea pia dawa ya majribio kutoka kwa shirika la afya duniani WHO, lakini haikubainika mara moja iwapo taarifa hiyo ilikuwa inamaanisha dawa ya ZMapp au nyingine.

Usalama na ufanisi wa ZMapp

Katika wiki chache zilizopita, dawa hiyo ya majaribio imetumiwa kwa wafanyakazi wawili wa misaada wa Marekani walioambukizwa ugonjwa huo wakifanya kazi kwenye hospitali ya wagonjwa wa Ebola. Siku ya Jumatatu, maafisa wa Uhispania walisema tiba hiyo ilikuwa imetumika kwa Padri mmishonari wa Kihispania alieuguwa akiwa nchini Liberia.

Wamarekani wanasemekana kupata nafuu, lakini hakuna njia yoyte ya kubainisha iwapo dawa hiyo imesaidia, au wanapata nafuu kivyao kama walivyopata nafuu wengine. Karibu asilimia 40 ya walioambukizwa virusi vya Ebola wananusurika mripuko wa sasa.

Mwandishi: Iddi ismail Ssessanga/ape,afpe,dpae.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi