1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya: Haftar atangaza 'vita vya mwisho' kuikomboa Tripoli

Daniel Gakuba
13 Desemba 2019

Kamanda wa vikosi vinavyodhibiti sehemu ya mashariki ya Libya, Khalifa Haftar ametangaza alichokiita, ''Vita vya mwisho'' vya kuukamata mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli, kutoka serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Libyen Symbolbild Regierungssoldat
Picha: picture-alliance/Photoshot

Kauli hiyo ya vita ameitoa Haftar akivalia nguo za kijeshi, katika kituo cha televisheni cha Hadath cha nchini Libya.

''Leo tunatangaza vita vikali vya kusonga mbele kuelekea kwenye kitovu cha Tripoli na kuukomboa mji huo, ili kuvunja minyororo na kuwaachia huru mateka wake, na kueneza furaha katika mioyo ya wakaazi wake.''  Amesema mbabe huyo wa kivita, na kuongeza kuwa ''Tripoli itarejeshewa nuru yake ya kihistoria, na kuwa tena mji mkuu wa utamaduni.''

Khalifa Haftar amesema imewadia saa ya operesheni kali, ambayo amedai kila mtu huru na mwenye heshima yake nchini Libya alikuwa akiisubiri kwa shauku kubwa.

Jenerali Khalifa Haftar (picha ya maktaba), mbabe wa kivita nchini LibyaPicha: picture-alliance/dpa/M. Elshaiky

Amesema vikosi anavyoviongoza vijulikanavyo kama jeshi la taifa la Libya, LNA kwa kifupi vitapata ushindi katika vita vya kuikomboa Tripoli, ambayo amedai imegeuzwa kuwa ''pango la wahalifu, ambamo watu hunyanyaswa kwa mtutu wa bunduki''.

Maaneo yaanza kukamatwa

Muda mfupi baada ya tangazo hilo la vita, chombo cha habari cha vikosi vyake kimesema vikosi hivyo vimechukua udhibii wa chuo cha kijeshi kusini mashariki mwa Tripoli katika mkoa wa Salah Eddin. Chombo hicho pia kimearifu kuwa mkoa mwingine wa Al-Tougar umeanguka mikononi mwa vikosi vitiifu kwa kamanda Khalifa Haftar.

Libya imekosa utulivu kwa muda wa miaka minane sasaPicha: AFP

Katika tangazo lake Haftar ameahidi kuwapa njia salama wapiganaji wa mjini Tripoli ikiwa watakubali kuweka chini silaha zao, na amevitaka vikosi vyake kuheshimu nyumba za wakaazi.

Jaribio la mwendawazimu 

Kwa upande mwingine, serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa imesema inadhibiti hali ya mambo mjini Tripoli, na kwamba jeshi lake lilikuwa likifanya doria katika maeneo ya Kusini mwa mji huo.

Waziri wa mambo ya ndani katika serikali hiyo Fathi Bashagha amesema wako tayari kurudisha nyuma kile alichokiita, ''jaribio lolote la kiwendawazimu kutoka kwa mbabe Haftar.''

Aprili mwaka huu, Khalifa Haftar aliamuru kampeni ya kijeshi ya kuukamata mji wa Tripoli kutoka serikali ya waziri mkuu Fayez al-Sarraj, lakini kwa wakati huu mgogoro huo ulikuwa katika hali ya mkwamo.

Libya imekuwa ikikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu kuangushwa kwa utawala wa muda mrefu wa dikteta Moamar Gaddafi mwaka 2011.

dpae, afpe

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW