Libya haitamkabidhi seif Al Islam kwa ICC
22 Novemba 2011Mohammed Allagui waziri wa sheria nchini Libya amesema kushtakiwa kwa Seif Al Islam ni jambo muhimu linalopaswa kufanywa na mahakama za Libya peke yake bila msaada wa taifa lolote. Allagui amesema hatua hii inapaswa kuheshimiwa na mataifa yote na kuwa hii inahusu uhuru wa Libya pamoja na raia wake.
Luis Moreno-Ocampo, amewasili hii leo nchini Libya kujadiliana na mamlaka nchini humo hatma ya Saif al Islam, mwanawe aliyekuwa kiongozi wa Libya, hayati Muammar Gaddafi, aliyekamatwa katika jangwa la kusini mwa nchi hiyo juma lililopita baada ya miezi mitatu mafichoni. Afisa mkuu wa ujasusi wa Gaddafi, Abdullah al-Senussi pia alikamatwa.
Saif al-Islam Gaddafi na Abdullah al-Senussi wote wanakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinaadamu, ikiwemo mauaji na mateso ya raia.
Allagui amesema Luis Ocampo anakaribishwa wakati wowote kuzungumza na Seif al Islam ili kuondoa wasiwasi kuwa huenda mwanawe Gaddafi anateswa mahali anapozuiliwa, katika milima ya Nafusa kilomita 170 kusini magharibi mwa Tripoli. Hata hivyo akizungumza na wanahabari Ocampo amesema kuwa kwa sasa hakupanga kuonana na Seif al Islam.
Baada ya mazungumzo yaliofanyika mjini Benghazi, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amesema amepokea hakikisho kuwa mwanawe Gaddafi hatateswa. Rice amesema maafisa ambao wanamzuilia Seif al Islam wamemwambia kuwa yuko salama na atashtakiwa bila kuhujumu haki zozote za kibinaadam na haki kutendwa ikizingatiwa mfumo wa juu wa kimataifa.
Kwa upande wake Ocampo amesema swala la Libya kuendesha kesi ni jambo ambalo litazungumzwa kwa undani zaidi na mahakama hiyo, kwa kuwa bado kuna vigezo muhimu vinavyopaswa kutiliwa maanani kabla ya kukubalika ni wapi kesi hiyo ifanyike.
Hata Hivyo baraza la kitaifa la mpito nchini Libya limetaka mwanawe Gaddafi kupelekwa Tripoli ambapo anatarajiwa kupewa hukumu ya kifo. Bado baraza hilo halijatoa maoni yake juu ya Senussi anayezuiliwa katika eneo la siri. Senussi hajawahi kuonekana tangu kukamatwa kwake.
Mahakama ya kimataifa ya jinai ilipokea ombi la kuendesha kesi nchini Libya chini ya azimio la umoja wa mataifa Februari 26 mwaka huu. Mahakama hiyo inajishughulisha na kesi za mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita, na uhalifu dhidi ya haki za kibinaadam, kesi hizi zinafanyika iwapo nchi husika hazina uwezo wa kuziendesha.
Mwandishi Amina Abubakar/AFPE
Mhariri Josephat Charo