Libya: Mchakato wa kisiasa unapaswa kuanzishwa mwaka ujao
9 Novemba 2018Ghassan Salame ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa viongozi wanne wa taifa hilo linalokumbwa na vita, walikubaliana mapema mwaka huu kuandaa uchaguzi wa urais na bunge mnamo Desemba 10, lakini kumekuwepo na uahirishwaji na masuala yanayokinzana tangu kukubaliwa kwa mpango huo.
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa Walibya wamechoka na hali mbaya ya kisiasa nchini mwao na kwamba bunge lao limewafelisha mara kwa mara.
"Raia wa Libya, Umoja wa Mataifa na jamii ya Kimataifa wametoa kila nafasi ya bunge kuchukua maamuzi kwa manufaa ya taifa la Libya. Lakini bunge hilo limeshindwa kutekeleza majukumu yake," alisema Salame.
Ghassan Salame kwa sasa ametoa wito wa kufanyika mkutano wa kitaifa katika wiki ya kwazana ya mwaka 2019 ikifuatiwa na mchakato wa uchaguzi katika majira ya machipuko huku akiangazia kura ya maoni inayoonesha asilimia 80 ya walibya wanasisitiza kuwepo uchaguzi wa haraka.
Mkuu wa serikali inayotambuliwa Kimataifa ahimiza kupata muelekeo wa pamoja juu ya mgogoro unaoikumba Libya
Huku hayo yakiarifiwa, mkuu wa serikali ya Libya inayoungwa mkono kimataifa, Fayez al Sarraj, ameihimiza jamii ya Kimataifa kupata muelekeo wa pamoja juu ya mgogoro ulioikumba nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Ameyasema hayo kuelekea mazungumzo ya kuujadili mgogoro huo utakaofanyika kisiwa cha Sicily nchini Italia wiki ijayo.
Katika mahojiano aliofanyiwa na shirika la habari la AFP katika makao makuu ya serikali ya mjini Tripoli, Sarraj amesema kuna mataifa yanayoiingilia vibaya Libya bila kutaja majina ya mataifa hayo.
Serikali ya Sarraj ya makubaliano ya kitaifa iliundwa chini ya mkataba wa mwaka 2015 ulioongozwa na Umoja wa Mataifa, lakini serikali hasimu iliyo mashariki mwa nchi hiyo imekataa kuitambua serikali ya hiyo.
Libya iliingia katika mgogoro wa kisiasa tangu alipoondolewa na kuuwawa kiongozi wa taifa hilo Muammar Gadaffi kwa msaada wa jeshi la Jumuiya ya Kujihami ya NATO lililounga mkono maandamano ya kutaka mageuzi yaliofanyika mwaka 2011, huku makundi hasimu yakigombania maeneo hasa yale yaliyo tajiri kwa mafuta.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef