1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya: Mkuu wa serikali inayotambuliwa na UN kujiuzulu

Daniel Gakuba
17 Septemba 2020

Waziri Mkuu wa serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa Fayez Serraj ametangaza nia ya kukabidhi madaraka kwa uongozi mpya mwezi Oktoba, wakati mazungumzo yakiendelea kusuluhisha mzozo nchini mwake.

Fajis al-Sarradsch Libyen
Waziri Mkuu wa Libya anayeondoka, Fayez SerrajPicha: Imago

''Natangaza nia yangu ya dhati ya kukabidhi hatamu za uongozi kwa baraza la utawala linalofuata, kabla ya mwezi Oktoba kumalizika'', ndivyo  alivyotangaza nia yake waziri mkuu Fayez Serraj katika hotuba kwa taifa lake kupitia televisheni usiku a kuamkia leo. Kiongozi  huyo amesema hali ya kisiasa na kijamii nchini Libya iko katika mivutano mikubwa, na hali hiyo inazitatiza juhudi za kutafuta suluhisho la kisiasa na kuepusha umwagikaji wa damu.

Soma zaidi:Ujerumani yaandaa mkutano wa kilele kutafuta amani ya Libya

Waziri mkuu huyo wa serikali ya mjini Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa amesema kuwa majadiliano ya hivi karibuni baina ya pande hasimu ambayo yalidhaminiwa na Umoja wa Mataifa, yameifikisha Libya katika kipindi kipya cha maandalizi ya kuziunganisha taasisi za kitaifa, na kusafisha njia kuelekea uchaguzi wa bunge na wa rais.

Muda muafaka wa kufunga virago

Kikao cha serikali ya umoja wa kitaifa mjini Tripoli, LibyaPicha: picture-alliance/AP Photo/GNA Media

Waziri Mkuu Fayez Serraj amesema kuwa ni katika mazingira hayo ya kuelekea uchaguzi,ambapo ananuia kuachia ngazi.

''Na kwa nukta hiyo, natangaza nia yangu ya dhati kukabidhi madaraka kwa utawala unaofuata, katika muda usiozidi mwezi ujao wa Oktoba,'' amesema Serraj na kuongeza huwa hadi wakati huo ''naamini kamati ya mazungumzo itakuwa imekamiisha kazi na kuchagua baraza jipya la utawala, na kiongozi mpya wa serikali, atakayepokea madaraka. Tunawatakia mafanikio, Mungu akipenda.''

Mkutano mwingine wa kilele kuhusu Libya

Wakati hayo yakiarifiwa, Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na serikali ya Ujerumani inatayarisha mkutano mwingine wa kilele kuhusu Libya, ambao utafanyika kwa njia ya video tarehe tano Oktoba, hilo likiwa ni kwa mujibu wa msemaji wa umoja huo mjini New York.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: Imago Images/Xinhua/

Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ataungana na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi kadhaa, pamoja wa wajumbe wa pande zinazohasimiana nchini Libya.

Hatua nyingine baada ya Berlin

Mkutano huo utakuwa ni mwendelezo wa mwingine uliofanyika mwezi Januari mjini Berlin, ukizishirikisha nchi zote zinazojihusisha katika mzozo wa nchini Libya.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya wataka pande hasimu nchini Libya kuweka silaha chini

Katika mkutano huo, nchi hizo zilikuwa zimeahidi kusimamisha kuyapa silaha makundi yanayopigana vita.

Wawakilishi wa Ujerumani, Umoja wa Mataifa, Marekani, Uingereza, Ufaransa, na China ni miongoni mwa watakaoshiriki katika mkutano huu wa Oktoba. Pande nyingine zitakazokuwa na wajumbe ni Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jamhuri ya Kongo, Italia, Misri na Algeria. Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia watahudhuria mkutano huo.

dpae, afpe

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW