1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLibya

Libya: Nchi isiyotawalika na kitisho kwa wahamiaji

15 Julai 2024

Biashara haramu ya kusafirisha binaadamu, wanamgambo na hata kugundulika kwa makaburi ya halaiki, yote haya hayawashtui wahamiaji waliodhamiria kwenda Libya.

Wahamiaji wenye asili ya Afrika wakiwa kwenye mpaka wa Libya na Tunisia
Wahamiaji wenye asili ya Afrika wakionekana kwenye mpaka wa Ras Ajdir unaozitenganisha Libya na Tunisia.Picha: Hazem Ahmed/REUTERS

Mnamo wiki iliyopita maafisa wa usalama waliuvamia mgahawa mmoja katika mji wa pwani wa Libya wa Zuwara, ulioko karibu na mpaka wa Tunisia ambako kundi kubwa la wahamiaji lilikuwa limepiga kambi kusubiri kuomba kazi. Watu hao ambao ni wanaume walikusanywa pamoja na kukamatwa. 

Michael Shira aliye na miaka 19, anaetokea Nigeria aliyekuwa pia katika mgahawa huo alikuwa na bahati ya kuponea kamata kamata iliyokuwepo huko.

Hata hivyo ameiambia DW kwamba wanaishi kwa hofu. Kwa sasa serikali ya Libya inawakamata wahamiaji popote pale inapowapata. Shira amekuwa akijificha nchini Libya kwa miezi kadhaa sasa akijaribu kupata kazi na pia kupata nafasi ya kupanda boti na kufika Ulaya.

" Kwanza nilikuwa Tunisia, lakini nikafukuzwa na polisi wa taifa hilo" alisema Shira ambaye baadae aliingia nchini Libya ambako pia katika mchakato huo alikuwa karibu akamatwe.

Makundi ya Haki za Binadamu yanasema wahamiaji wanakabiliwa na matatizo lukuki ikiwemo vitendo vya unyanyasaji. Picha: Hazem Ahmed/REUTERS

Liz Throssellni msemaji wa ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, ameiambia DW kwamba wanaendelea kushuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki hizo kwa wahamiaji, wakimbizi na waomba hifadhi.

Kulingana na Umoja wa Mataifa ukiukwaji huo unajumuisha usafirishaji haramu wa watu, mateso, kulazimishwa kufanya kazi ngumu, baadhi kunyimwa chakula katika vituo wanavyozuiliwa, vitisho na kundolewa kwa nguvu nchini humo.

Amesema haya yote yanafanyika kwa wingi na uwepo wa kinga kwa viongozi wa ndani na nje ya nchi wanaotekeleza yote haya kwa ushirikiano mkubwa na kwa siri na baadhi ya maafisa na haya ni mambo yanayofanya hali kuwa mbaya zaidi.

Kamishna wa Haki wa UM atoa wito wa uchunguzi baada ya kupatikana makaburi ya halaiki 

Kwa upande wake Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Binaadamu, ameuhimiza utawala wa Libya kuanza uchunguzi wa haraka kuhusu upatikanaji wa hivi karibuni wa kaburi la pamoja karibu na mpaka wa Libya na Tunisia, pamoja na kaburi jengine pia la pamoja lililopatikana katika eneo la milima la Al Jahriya mwezi Machi mwaka huu lililokuwa na miili 65.

Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Binaadamu.Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Katika miaka ya hivi Karibuni Libya na Tunisia mataifa yaliyo kaskazini mwa Afrika yamegeuka kuwa njia ya wahamiaji kutoka eneo la sahara kuingia Ulaya. Mataifa yote mawili yanashirikiana na Umoja wa Ulaya inayotaka kudhibiti ujio wa wahamiaji katika bara hilo kupitia bahari ya Mediterenia.

Kupungua kwa safari za kufikia Ulaya hakumaanishi kwamba watu wachache wanasafiri kwenda Libya. Makundi ya kutetea haki za binaadamu yanaripoti kuongezeka kwa safari hizo lakini yakatahadharisha kwamba idadi kamili haijulikani kwa sababu ya Libya kuwa katika mkwamo wa kisiasa kwa miongo kadhaa sasa.Eneo la Magharibi mwa Libya linaongozwa na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa iliyo chini ya uongozi wa rais Abdul Hamid Dbeibah mjini Tripoli huku serikali ya Mashariki ikiwa chini ya uongozi wa jenerali Khalifa Haftar. Hali ya kisiasa imekuwa mbaya zaidi kutokana na machafuko na wanamgambo kutawala katika maeneo mengine ya nchi.Kukosekana kwa sheria na utulivu wa kisiasa nchini humo na kuendelea kufanya kazi kwa mitandao ya kimagendo kwa ushirikiano wa baadhi ya maafisa kunamaanisha bado safari kama hizo zinaendelezwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW