1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yaendelea kukabiliwa na machafuko miaka 10 baadae

10 Februari 2021

Miaka 10 baada ya vuguvugu la mapambano ya Walibya kumuondowa madarakani na kumuua kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Moammer Ghaddafi, nchi hiyo bado iko katika dimbwi la matatizo, migogoro na vurugu.

Schweiz Libysches Dialogforum in Genf
Picha: UNITED NATIONS/AFP

Libya ina utajiri mkubwa sana wa mafuta lakini pia ni nchi iliyotumbukia katika umasikini mkubwa miongoni mwa wananchi wake. Ni kutokana na vita na vurugu zinazoendelea kushuhudiwa kila kukicha.

Lakini pia hali hiyo ya vita imeigeuza nchi hii kuwa kitovu kikubwa Afrika Kaskazini  cha biashara haramu ya usafirishaji binadamu ambapo makumi kwa maelfu ya wahamiaji hujaribu bahati yao kupitia Libya kwa kutumia njia za hatari kabisa za kuvuka kwa maboti kuvuka kuingia Ulaya.

Soma pia: Libya yapata serikali ya mpito

Ripoti zinazosimulia hadhithi za kutisha za wakimbizi kuzama katika bahari ya Mediterania ni miongoni mwa mambo yanayothibitisha pia ripoti nyingine za kutisha kuhusu unyanyasaji na mateso wanayopata wahamiaji hao mikononi mwa wanamgambo wanaosimamia kambi za kuwashilikilia wafungwa  nchini humo.

Walibya wakiwa katika mkutano wa kuchagua viongozi wa mpito kuelekea uchaguzi unaotazamiwa kurejesha utulivu nchini humo.Picha: UNITED NATIONS/AFP

Libya imekuwa nchi ambayo pia yanagundulika makaburi yaliyozikwa watu wengi waliouwawa katika vita vya karibuni. Kwa hali hii sura halisi ya Libya inayoonekana wazi, miaka kumi baada ya  mapinduzi ni kwamba vuguvugu hilo limeishushia balaa nchi hiyo badala ya uhuru na maendeleo walibya waliyotamani kwa muda mrefu kuyaona. Kwa walibya kama Jalel Harchaoui,afisa mwandamizi kutoka shirika la kimataifa la Global Initiative anasema.

"Katika kiwango cha utendaji wa kiufundi ikiwa tutaliangalia suala la idadi ya walibya wanaouliwa kila siku,ni kwamba idadi imepungua. Na watu ninaowazungumzia hapa ni wale wanaouliwa kila siku katika operesheni za kijeshi. Imepungua tangu mwezi Juni. Sasa unapokuja upande wa kisiasa, je tumepiga hatua yoyote? Je tumeondoka kwenye matatatizo?bila shaka jibu ni hapana,'' anasema Harchaoui.

Wakumbuka maisha ya zamani

Kuna simulizi nyingi za Walibya walioko ndani ya nchi hiyo kuhusu maisha yao ya kila siku katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.Majdi ni daktari wa meno ana umri wa miaka 36 yeye anakumbuka jinsi vuguvu la mapambano lilivyoanza huko Benghazi mashariki ya Libya Februari 2011 anasema wakati huo ndipo alipofahamu walikuwa wakiishi kwenye ugaidi bila ya kutambua.

Kaimu mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Stepanie Williams.Picha: UNITED NATIONS/AFP

Kilichoshuhudiwa Libya wakati huo ni mapambano kweli kweli ya makundi ya Walibya wakiungwa mkono na Jumuiya ya kujihami ya Nato iliyoshambulia kwa mabomu kutoka angani.Jumuiya ya Nato katika vita hii iliongozwa na Marekani,Uingereza na Ufaransa na hatimae utawala wa Gaddafi ukaangushwa na kiongozi huyo akauliwa kwa fedheha baada ya kuchomolewa kutoka kwenye bomba la maji taki alikokuwa amejificha.

Soma pia: Muda wa kuondoka vikosi vya kigeni nchini Libya wamalizika

Mwisho wa miaka 42 ya udikteta wa Gaddhafi ulichochea ghasia kubwa na vita vilivyosababisha silaha chungunzima pamoja na wapiganaji  kuingia Libya na kwa miaka sasa nchi hiyo ya watu milioni 7 inaendeshwa na makundi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na pande mbali mbali. Jalel Harchaoui anasema nchi mbali mbali za kigeni zimejikuta zikiingizwa katika vita ya Libya.

"Kwasababu nchi za Magharibi zilijiingiza toka mwanzo,nchi ambazo sio za magharibi  kama Qatar,Emarati,Misri na bila shaka Urusi  ambazo kwa kiasi fulani zilipuuzwa mwaka 2011 na zilipoteza fedha nyingi, zililazimishwa na nchi hizo za Magharibi kujiunga kwenye vita na wakakubali kupoteza raia wao. Uturuki kwa mfano ilipoteza wanajeshi wake mwaka 2020.''

Watu 30 wauawa Libya kwa mabomu ya ardhini

00:56

This browser does not support the video element.

Soma pia: UN: Libya ina wapiganaji 20,000 wa kigeni na mamluki.

Libya hivi sasa imegawika kambi mbili zinazopingana moja ikiwa Tripoli  na nyingine iko mashariki kila upande ukiwa na mamlaka yake. Serikali iliyoko Tripoli ambayo inatambuliwa kimataifa iliundwa mwaka 2016 na upande wa Mashariki ipo serikali inayotambuliwa na bunge ambayo inaongozwa na jenerali wa kijeshi Khalifa Khaftar.

Umoja wa Mataifa unawataka Walibya wenyewe kuamua mustakabali wao lakini mpaka sasa hakuna makubaliano yanayoonesha kuwa na ishara ya kufanikiwa bila kwanza ya nchi za kigeni zilizoingia kwenye vita hiyo,kwa kupeleka wanajeshi wao, kuyafikia makubaliano hayo.

Chanzo: Mashirika

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW