Libya yaonywa kuhusu ufisadi na usafirishaji haramu wa watu
22 Mei 2018Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya Ghassan Salame ameionya nchi hiyo kuwa mfumo wake wa kiuchumi unaojikita katika ufisadi na kusafirisha watu na bidhaa kwa njia haramu unapaswa kuvunjiliwa mbali ili kukomesha mzozo wa kisiasa na Libya kupiga hatua kuelekea uthabiti na kuandaliwa kwa chaguzi za kidemokrasia mwaka huu.
Baada ya Salame hapo jana kuyasema hayo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amefichua kuwa baraza hilo lenye wanachaam 15 linatafakari kuwaweka viongozi sita wa Libya wanaohusishwa na mtandao wa usafirishaji wa watu kwa njia za kimagendo katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa.
Salame pia ameonya kuwa kuendelea kwa makundi ya wapiganaji kuwa na ushawishi katika masuala ya kisiasa na kiuchumi ni jambo hatari na lisipoepukwa kuna hatari ya kusambaa zaidi kwa msukosuko unaoikumbwa Libya.