1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yatanda maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya23 Februari 2011

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya hali ya nchini Libya na juu ya kashfa ya waziri wa ulinzi zu Guttenberg.

Muammar Gaddafi
Muammar GaddafiPicha: picture alliance/dpa

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya hali ya nchini Libya.

Mhariri wa gagzeti la Reutlinger General -Anzeiger anasema jambo moja ni la uhakika, kwamba yanayotokea nchini Libya ni matukio ya kutia wasiwasi duniani kote. Gazeti hilo linaeleza kuwa huenda mtu akafikiri ,kuwa ni kupiga chuku kusema hayo, kutokana na Libya kuwa nchi ya watu milioni sita tu. Lakini anasema Libya inatoa mchango muhimu katika uchumi wa dunia kutokana na utajiri wake wa mafuta.

Gazeti linasema sasa tayari pana miyumbiko kwenye masoko ya hisa kutokana na matukio ya nchini Libya.

Gazeti la Berliner Zeitung linachambua hali ya nchini Libya kwa kulizingatia suala la wakimbizi, lakini wakati huo huo linakumbusha juu ya usuhuba uliokuwapo hapo awali baina ya Umoja wa Ulaya na madikteta wa kaskazini mwa Afrika.Gazeti hilo linasema usuhuba na akina Gaddafi na Ben Ali ulikuwa ni jambo la fedheha. Sera za nchi za Ulaya za wiki zilizopita zilithibitika kuwa aibu. Lakini sasa upepo wa mabadiliko unavuma katika nchi za kiarabu-upepo unaoweza kusababisha wimbi la wakimbizi katika nchi za jirani. Kwa hiyo inalazimu sasa kuchukua hatua za haraka katika kutambua kwamba demokrasia kaskazini mwa Afrika maana yake ni kushirikiana na watu wa sehemu hiyo.

Gazeti la Dresdener Neueste Nachrichten pia linazungumzia juu ya suala la wakimbizi kutokana na mabadiliko yanayotokea kaskazini mwa Afrika. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba mkono wa Gaddafi haupo kwenye bomba la mafuta tu. Lakini Gaddafi pia ameushika ufunguo wa lango la kuingilia Ulaya kwa mamilioni ya wakimbizi.

Gazeti la Financial Times Deutschand linaupongeza msimamo wa serikali ya Ujerumani juu ya matukio ya nchini Libya. Gazeti hilo linafafanua kwa kusema kuwa Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Westerwelle amechukua hatua sahihi kwa kuvunja mwiko wa kidiplomasia. Ujerumani inajiingiza katika mambo ya ndani ya Libya na kusimama katika upande wa wapinzani wa serikali.


Gazeti la Nordwest- Zeitung linatoa maoni juu ya kashfa inayomhusu waziri wa ulinzi wa Ujerumani Karl-Theodor zu -Guttenberg

Waziri huyo aliingiza kazi za waandishi wengine katika tasnifu yake ya udakta bila ya kutaja hisani ya waandishi hao.

Waziri huyo amejitetea kwa kusema kuwa alikuwa chini ya shinikizo kubwa la kazi.

Lakini mhariri wa Nordwest hakubaliani na hoja hiyo.Na anauliza ni nani anaeandika tasnifu bila ya kutingwa na kazi nyingi?

Mwandishi/MtullyaAbdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW