1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yatishia kuzama katika Bahari ya Vurugu na Vita

22 Oktoba 2014

Waziri mkuu anaeongoza serikali ambayo haitambuliwi na jumuia ya kimataifa nya Libya amekutana na mjumbe wa Uturuki katika wakati ambapo mapambano yanapamba moto Tripoli na pia katika mji wa mashariki wa Benghazi.

Mapigano yaliyoripuka Benghazi kati ya vikosi tiifu kwa jenerali Khalifa Hifter na wanamgambo wa itikadi kaliPicha: picture-alliance/AP Photo/Mohammed el-Sheikhy

Madola ya magharibi na majirani wa Libya wanahofia mzozo huo unaweza kuitumbuliza nchi hiyo ya Afrika kaskazini katika vurugu au hata kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na ile hali kwamba waasi wa zamani waliosaidia kumpindua Muammar Gaddafi ndio wanaopigana kuania madaraka hivi sasa.

Waziri mkuu Omar al Hasi anaeongoza serikali mjini Tripoli amekutana na mjumbe maalum wa Uturuki Emrullah Isler ambae hapo awali aliitembelea pia serikali inayotambuliwa kimataifa na kuongozwa na Abdullah al Thinni,iliyoko Tobruk- linakokutikana pia bunge,mashariki ya nchi hiyo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uturuki amekwepa kutoa maelezo yoyote kuhusu ziara ya mjumbe huyo maalum.

Wakati huo huo mapigano yamepamba moto magharibi ya Tripoli vikosi vinavyoelemea upande wa serikali vikijaribu kuukomboa mji mkuu Tripoli kutoka mikononi mwa waasi na kuwataka wananchi wasiitii serikali hiyo.

Vikosi vya serikali hlali vinajitahidi kusonga mbele

Kwa mujibu wa ripota wa shirika la habari la Ufaransa ,AFP silaha nzito nzito na makombora yametumika katika mapigano hayo karibu na mji wa Kekla ulioko umbali wa kilomita 120 kusini mashariki ya mji mkuu ambako vikosi tiifu kwa serikali vinajitahidi kusonga mbele.

Moshi unafuka toka makao makuu ya wanamgambo wa Qaqaa kufuatia mapigano kati ya makundi hasimu ya wanamgambo mjini TripoliPicha: Reuters

Kwa mujibu wa meya wa Kekla,Noureddine Meftah,zaidi ya watu 100 wameuliwa na 300 kujeruhiwa katika mapigano hayo yanayoendelea tangu Octoba 11 iliyopita.

Jana waziri mkuu al Thinni alisema serikali yake inatafuta misaada ili kuwavunja nguvu wanamgambo wanaoidhibiti miji muhimu ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na mji mkuu Tripoli.

Al Thini alikuwa Malta ambako aliongoza ujumbe akiwemo naibu wake na mwaziri wake wanne.

Juhudi za upatanishi zimshika kasi

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Libya Bernardino Leon alitrajiwa kuwasili Malta kwa mazungumzo pamoja na Al thinni kuhusu juhudi za kumaliza mzozo unaoigubika nchi hiyo ya Afrika kaskazini.

Waziri mkuu Abdullah al Thinni akihudhuria mkutano na waandishi habari pamoja na waziri mkuu wa Malta Joseph Muscat(hayumo ndani ya picha).Picha: Reuters

Akiulizwa katika mkutano na waandishi habari kama ataunga mkono mataifa ya kigeni yaingilie kijeshi nchini Libya,waziri mkuu Al Thinni amesema serikali yake inatafuta msaada wa kimbinu tu.

Ziara ya waziri mkuu wa Libya na mawaziri wanne wa serikali yake nchini Malta inafungamanishwa na juhudi za upatanishi kumaliza mzozo huu wa sasa uliopelekea serikali liyochaguliwa na umma kupoteza udhibiti wa mji mkuu Tripoli na miji mengine muhimu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman