1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Licha ya ahadi ya Taliban kutolipiza kisasi, maelfu waondoka

18 Agosti 2021

Zaidi ya wanadiplomasia 2,200 na raia wamehamishwa kutoka Afghanistan kwa ndege za kijeshi wakati juhudi za kuwahamisha watu zikiendelea kushika kasi kutokana na wasiwasi juu ya utawala wa Taliban.

Usbekistan Taschkent | Ankunft Evakuierungsflug aus Kabul
Picha: Bundeswehr

Kundi la Taliban limesema linataka amani, na limeahidi kuwa halitalipiza kisasi dhidi ya maadui zao wa zamani. Kundi hilo pia limesema litaheshimu haki za wanawake kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Hata hivyo licha ya ahadi zote hizo, maelfu ya Waafghani hasa wale waliofanya kazi kwa ushirikiano na vikosi vya usalama vya kimataifa kwa zaidi ya miongo miwili, wanapanga kuondoka nchini humo.

Afisa wa usalama wa mataifa ya Magharibi amesema na hapa namnukuu, "Tunaendelea kwa kasi kubwa na juhudi za kuwahamisha watu, hadi sasa hatujapata changamoto zozote na tumefanikiwa kuwahamisha zaidi ya wafanyikazi 2,200 maafisa wa usalama na Waafghani waliofanya kazi katika ofisi za ubalozi.

Soma zaidi: UN: Waafghanistan wasilazimishwe kurudi nchini mwao

Afisa huyo hata hivyo hakueleza ni lini safari za ndege za umma zitakapoanza. Pia hakuweza wazi idadi ya raia wa Afghanistan waliokuwepo kati ya watu hao 2,200 waliohamishwa kwa kutumia ndege ya kivita ya Marekani ya kubebea mizigo.

Uingereza yaahidi kufanya kila liwezekanalo kuepusha mzozo wa binadamu

Taliban wakishika doria katika eneo la Wazir Akbar Khan, mjini KabulPicha: Rahmat Gul/AP Photo/picture alliance

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Priti Patel amesema tayari Uingereza imewahamisha watu wapatao 1,000 wakati Waziri Mkuu Boris Johnson akiahidi kufanya kila liwezakano kuepusha mzozo mbaya wa kibinadamu nchini Afghanistan.

"Tutafanya kila juhudi kuwasaidia wale waliousaidia ujumbe maalum wa Uingereza nchini Afghanistan, na pia tutasaidia kwa kila hali eneo pana la Afghanistan ikiwemo kuzuia mzozo wa kibinadamu. "

Baada ya Taliban kuchukua usukani, afisa mwandamizi wa kundi hilo amesema mmoja kati ya viongozi na waanzilishi wake Mullah Abdul Ghani Baradar amerudi nchini humo kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa zaidi ya miaka 10.

Afisa huyo mwandamizi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, viongozi wa Taliban watajitokeza kwa macho ya ulimwengu tofauti na miaka ya nyuma, ambapo walikuwa wakiishi kwa usiri mkubwa.

Soma zaidi: Licha ya kukosolewa, Biden atetea uamuzi wa kuondoa vikosi Afghanistan

Wakati hayo yakiarifiwa, kundi hilo limeilipua sanamu ya kiongozi wa dhehebu la Kishia aliyepambana na Taliban wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Afghanistan katika miaka ya 90.

Sanamu ya Abdul Ali Mazari, mbabe wa kivita aliyeuawa na Taliban mnamo mwaka 1996 wakati wanamgambo hao walipochukua madaraka kutoka kwa wapinzani wao ililipuliwa.

Mazari alikuwa kiongozi wa wasilamu wachache wa madhehebu ya Kishia waliopitia mateso makubwa chini ya utawala wa Taliban, waislamu waliokuwa wengi wa madhehebu ya Sunni.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW