Licha ya hali ngumu, Scholz aapa kupambana hadi mwisho
13 Januari 2025Sehemu kubwa ya wajumbe 600 wa mkutano mkuu wa chama hicho kinachofuata siasa za mrengo wa kushoto kati walimthibitisha Kansela Scholz kuwa mgombea wao kwa uchaguzi wa bunge unaofanyika mwezi ujao.
Mkutano huo ulifanyika siku ya Jumamosi (Januari 11) katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.
Mseto wa SPD, Walinda Mazingira wa Kijani na waliberali mambo leo wa Free Democrats (FDP) ulishindwa vibaya mwishoni mwa mwaka 2024, hali iliyofuatiwa na kura ya kutokuwa na imani na bungeni iliyopelekea uchaguzi wa mapemba uliopangwa kufanyika Februari 23.
Soma:Scholz apinga wito wa kuongeza bajeti ya ulinzi ya NATO
Hivi sasa, kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya wapiga kura ulioandaliwa na kituo cha utangazaji cha ARD, asilimia 77 ya Wajerumani hawaridhishwi na uongozi wa Scholz, na kwa wiki kadhaa SPD ilikuwa inajadili endapo wamchaguwe mmoja wa wanachama wao mashuhuri kuongoza kampeni.
Scholz, mwanasiasa mwenye umri wa miaka 66, anapenda kujionesha kuwa mtu anayejiamini anayekwepa kutegemea utafiti wa maoni ya wapigakura.
Inavyoonekana hakukereka sana na wasiwasi wa wenzake.
Tayari kwa mapambano
Ingawa hatima yake ya kisiasa iko hatarini, Scholz alionekana mtu mwenye kujiamini na tayari kwa mapambano kwenye mkutano huo mkuu wa chama chake.
Endapo SPD itapoteza uchaguzi wa bunge wa Februari 23 kama utafiti wa maoni ya wapigakura unavyoonesha, muda wa miaka mitatu aliyokaa madarakani Scholz, utakuwa ndio mfupi zaidi kwenye historia ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.
Soma zaidi: Vyama vikuu Ujerumani vyazindua kampeni kuelekea uchaguzi
Kwa sasa, SPD ina chini ya nusu ya uungaji mkono ambao wapigakura wanauonesha kwa vyama ndugu vya CDU na CSU.
Lakini kuna mengi yanayoweza kutokezea baina ya sasa na hapo Februari 23, kama wanachama wa SPD wanavyopenda kujipumbaza.
"Ni kipindi muhimu kwelikweli, muda ambapo mambo makubwa yanayotokea. Haya ni mambo ambayo hakuna aliyewahi kudhani yangelitokea miaka michache ijayo, ama pengine hata miezi au wiki chache zilizopita." Alisema Scholz kwenye mkutano mkuu wa SPD.
Msukumo kutoka siasa za kimataifa
Miongoni mwa hayo aliyoyakusudia Scholz ni la Donald Trump kurejea kwenye Ikulu ya White House, Marekani.
Ifikapo Januari 20, bilionea huyo wa Kimarekani ataapishwa wakati tayari akiwa ameshaanza kuzusha tafrani duniani, pale alipotowa madai ya kuzitwaa Greenland, Canada na Mfereji wa Panama.
Soma zaidi: Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani atarajia mahusiano mazuri na serikali mpya Marekani
Pia alitowa madai makubwa akitaka kila mwanachama wa Muungano wa Kijeshi wa NATO kuchangia asilimia 5 ya mapato yao ya kiuchumi kwenye ulinzi, katika wakati ambapo ni thuluthi mbili tu ya wanachama hao wanaoweza kutimiza asilimia mbili waliyopangiwa kwa sasa.
Sarakasi za Trump zinaweza kumpa Scholz fursa kwenye kampeni za uchaguzi. Kwenye mkutano mkuu wa chama, aliyakataa tena madai ya Trump, akisema: "Kanuni ya kutoingilia mipaka inaihusu kila nchi, ama iwe mashariki au magharibi yetu. Kila dola lazima iiheshimu kanuni hii. Hakuna nchi ambayo ni uwani kwa nyengine. Hakuna nchi ndoyo inayopaswa kumuhofia jirani yake mkubwa. Hiki kiko kwenye kiini cha kile tunachokiita maadili ya Magharibi, maadili yetu."
Kwa wengine, hotuba hii ilikuwa ni ukumbusho wa mwaka 2003, pale Kansela Gerhard Schröder kupitia chama cha SPD alipopingana na uvamizi wa Iraq ulioendeshwa na Rais George W. Bush wa Marekani.
Upinzani huo wa Schröder ulimpatia uungaji mkono wa kutosha uliomletea ushindi wa kushangaza kwenye uchaguzi wa Bundestag.
Wanachama wa SPD wanajuwa kuwa masuala ya kimataifa yanaweza kuwa magumu zaidi baada ya Trump kuapishwa, na hilo linaweza kumbeba Scholz.