1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Tigray inaadhimisha mwaka mmoja wa mkataba wa amani

Angela Mdungu
2 Novemba 2023

Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limesema mapigano na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu vinaendelea kaskazini mwa Ethiopia mwaka mmoja baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya usitishaji wa mapigano.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed AliPicha: Massimo Percossi/Ansa/ZUMA Press/IMAGO

Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limesema mapigano na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu vinaendelea kaskazini mwa Ethiopia mwaka mmoja baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya usitishaji wa mapigano. Makubaliano hayo yalisainiwa na pande kuu mbili za mzozo huo mjini Pretoria Afrika ya Kusini Novemba 2 mwaka uliopita, hatua iliyoashiria mwisho wa mapigano huko Tigray.

Msaidizi wa mkurugenzi wa shirika la Human rights watch barani Afrika Leticia Bader amesema wakati serikali ya Ethiopia na washirika wake wa kimataifa wakijivunia hatua kubwa iliyopigwa katika mwaka huo mmoja, raia katika maeneo yenye mzozo wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa ukatili.

Soma zaidi: Tigray baada ya vita: Je, kuna nafasi ya amani?

Makubaliano ya Novemba 2022 yanaainisha hatua muhimu za kuwalinda raia, kuendelea kutolewa kwa huduma muhimu, kutolewa kwa misaada ya kiutu bila vikwazo na kuwawezesha wakimbizi wa ndani kurejea makwao pamoja, na kutekeleza dhamira ya serikali ya nchi hiyo ya kutengeneza sera ya haki. Sera hiyo inaalenga kudumisha uwajibikaji, haki, ukweli, upatanishi na uponyaji.

Pande hizo mbili zilikubaliana pia kuanzisha utaratibu wa ufuatiliaji wa makubaliano hayo ndani ya Umoja wa Afrika. Hata hivyo juhudi za Umoja wa Afrika zimejikita zaidii kuwanyang'anya silaha wapiganaji wa Tigray na haujumuishi waangalizi wa kufuatilia haki na masuala ya kijinsia au kuripoti kuhusu ukiukwaji wa makubaliano.

Pande hasimu zatuhumiwa kwa kuendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha uhasama

Katika mwaka mmoja uliopita, pande mbili za mzozo huo zimeendelea kukiuka haki Tigray kinyume cha makubaliano ya mwezi Novemba zilipoahidi kuwalinda raia, kulingana na taarifa ya Human Rights Watch. Taarifa hiyo imeeleza kuwa vikosi vya Eritrea vimefanya mauaji, unyanyasaji wa kingono, utekaji nyara,  uporaji  vimezuia misaada ya kiutu na kukwamisha kazi za wafuatiliaji wa  Umoja wa Afrika  katika maeneo vinayoyadhibiti.

Jengo la utawala wa TigrayPicha: Million Haileselassie/DW

Katika ukanda wa magharibi mwa Tigray, ambao kwa kiasi kikubwa haufikiwi na mashirika ya misaada ya wahisani, mamlaka na wanajeshi wa Amhara pamoja na wanamgambo wajulikanao kama Fano wameendelea na kampeni yao ya safisha safisha ya kikabila na kuwafukuza kwa nguvu watu wa Tigray.

Vita hivyo vilivyoibuka kaskazini mwa Ethiopia mwaka mmoja uliopita vimesababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao huku wengi wao wakiwa na uhitaji mkubwa wa misaada ya kiutu ikiwa ni matokeo ya mzingiro wa miaka miwili katika mkoa wa Tigray. Ingawa huduma muhimu ilianza kurejea na misaada ilianza kupelekwa Tigray katika miezi iliyofuata baada ya makubaliano ya kusitisha uhasama, huduma za kibenki na nyinginezo zimeendelea kukosekana katika  maeneo mengine ya Tigray tangu mwezi Oktoba mwaka huu.