Licha ya sheria dhidi ya ushoga Ujerumani itaisaidia Uganda
27 Februari 2014Hata hivyo hakuna uwezekano wa kupunguzwa misaada ya maendeleo kwa nchi hiyo ya Afrika mashariki.
Kwa mara nyingine tena taarifa za mashoga nchini Uganda zimegonga vichwa vya habari duniani. Gazeti moja nchini Uganda linalojulikana kama "Red Pepper" , Pilipili nyekundu , limechapisha Jumanne wiki hii taarifa pamoja na picha za watu 200 wanaoshukiwa kuwa mashoga.
Na hatua hiyo ilianzisha nchini humo msako wa kile tunachoweza kusema ni msako dhidi ya wahalifu. Usiku wa Jumatano mashoga wawili wanaoishi pamoja walishambiliwa , ameeleza mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Uganda Jacqueline Kasha. Mmoja kati ya mashoga hao amefariki na mwingine yuko hospitalini.
Wanaharakati
Hali hii inatuweka katika hali ya tahadhari. Miaka mitatu iliyopita mwanaharakati wa kutetea mashoga ambaye hakuwa akifahamika sana David Kato aliuwawa kinyama , na baada ya hapo gazeti moja lilichapisha picha yake. Kabla ya kifo chake Kato alilipeleka mahakamani gazeti moja , akidai kuwa mashoga wasidhalilishwe.
Hisia hizi kali dhidi ya mashoga hazishangazi hata hivyo.
Siku ya Jumatatu wiki hii rais wa Uganda Yoweri Museveni alitia saini mswada wa sheria unaosema kuwa mashoga na wale wanaotaka kufanya mahusiano na mashoga wataadhibiwa , na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Watetezi wa haki za binadamu pamoja na wanasiasa wameonya, kuwa hatua hiyo inaweza kuwaathiri kwa kiasi kikubwa mashoga nchini Uganda.
Wanasiasa duniani kote wamechukua hatua dhidi ya utiaji saini wa sheria hiyo.
Jumuiya ya kimataifa yapinga
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon , ameitaka Uganda kuheshimu na kuwalinda raia wote wa nchi hiyo dhidi ya ubaguzi na matumizi ya nguvu.
Ana matumaini kuwa sheria hiyo itafanyiwa mabadiliko ama kufutwa kabisa. Denmark , Norway na Uholanzi zimeeleza kuwa zinapunguza misaada yake ya maendeleo kwa Uganda. Sweden na Marekani pia zinatafakari hatua kama hizo.
Hata wanasiasa nchini Ujerumani wameonesha kushangazwa kwao. Adhabu kubwa kama hiyo haikubaliki, amesema afisa anayehusika na haki za binadamu katika serikali ya Ujerumani kutoka chama cha SPD Christoph Strässer.
"Kwetu sisi hili ni wazi kabisa, kuwa adhabu ya juu kama hiyo haikubaliki. Wanakiuka haki za kimataifa na pia wanakwenda kinyume na mikataba ya kimataifa, ambayo Uganda binafsi imetia saini."
Strasser binafsi anataka sheria hiyo ifutwe. Lakini Uganda si nchi peke yake ambayo ina sheria kama hiyo. Kenya, Tanzania na Sudan kusini pia zimepitisha sheria kama hiyo. Katika mataifa ya Afrika magharibi Nigeria pia imepitisha sheria kama hiyo.
Mwenyekiti wa kamati ya bunge inayohusika na masuala ya ushirikiano wa maendeleo Dagmar Wöhrl amesema hata hivyo madai ya watetezi wa haki za binadamu kuwa usitishwe ushirikiano na mataifa hayo si sahihi, kwa kuwa watakaoathirika ni watu wasio na uwezo na masikini.
Mwandishi: Philipp Sandner / ZR / Kitojo Sekione
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman