1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lieberman avunja ushirikiano na Likud

Mohamed Dahman8 Julai 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman ameuvunja ushirika wa kisiasa wa miezi ishirini wa chama chake na chama tawala cha Likud nchini Israel juu ya kwamba chama chake kitaendelea kubakia kwenye serikali.

Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman (katikati) katika mkutano na waandishi wa habari Jerusalem.(07.07.2014)
Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman (katikati) katika mkutano na waandishi wa habari Jerusalem.(07.07.2014)Picha: Reuters

Uamuzi huo umetangazwa katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu (07.07.2014) kufuatia mzozo mkubwa kati ya Lieberman na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kutokana na jinsi serikali inavyokabiliana na kuongezeka kwa mashambulizi ya maroketi ya wanamgambo wa Kipalestina dhidi ya Israel kutoka Ukanda wa Gaza.

Lieberman kiongozi wa chama cha sera kali za kizalendo cha Yisrael Beitenu ameuambia mkutano huo kwamba yeye na Netanyahu wana tafautiana sana katika masuala mengi muhimu na haingii tena akilini kuendedelea kuwa na ushirika baina vya vyama vyao.

Amesema " Kwa bahati mbaya tafauti za maoni kati yangu na waziri mkuu zimekuwa kubwa na haziruhusu kuendelea kuwa na ushirika wa kisiasa.Ukweli ni kwamba ushirika huo haukuweza kufanya kazi wakati wa uchaguzi na hadi hii leo kuna masuala ya kiufundi ambayo yanapogeuka kuwa matatizo ya msingi hakuna haja ya kuyaficha. "

Dhamira ya ushirika wao

Lieberman aliunda kundi la kushirikiana katika uchaguzi na chama cha Netanyahu cha Likud hapo mwezi wa Oktoba mwaka 2012 kabla ya uchaguzi wa mwezi wa Januari mwaka 2013 hatua ambayo wamesema itawawezesha kukabiliana vizuri zaidi na changamoto za usalama za Israel.

Wapalestina katika makabiliano na polisi wa Israel katika kitongoji cha Shuafat.(03.07.2014)Picha: Getty Images

Kundi hilo jipya lililopewa jina la Likud Beitenu lilipata ushindi wa wingi mchache wa kura kwa kujipatia viri 31 kati ya 120 vya bunge la Israel la Knesset ikiwa ni viti 12 tu zaidi kuliko mpinzani wake wa karibu chama cha sera za wastani cha Yesh Atid.

Kiini cha mzozo

Hivi karibuni kabisa viongozi hao walizozana juu ya jinsi ya kukabiliana na wimbi la mashambulizi ya maroketi dhidi ya Israel yanayotokea Ukanda wa Gaza.Netanyahu ametaka zichukuliwe hatua zenye uwiano wakati Lieberman amesema angependelea kuwepo na operesheni kubwa ya kijeshi kulitokomeza kundi la wanamgambo wa Hamas lenye kutawala Gaza jambo ambalo lingeliweza kupelekea maafa makubwa kwa pande zote mbili.

Jeshi la Israel katika mojawapo ya operesheni zake karibu na Ukingo wa Magharibi.Picha: Reuters

Uamuzi huo wa Lieberman aliouchukuwa leo hautowi tishio la moja kwa moja la uwepo wa serikali ya mseto wa Israel lakini hana haja tena ya kuratibu hatua zake na Netanyahu jambo ambalo itazidi kumuiya vigumu kwa waziri mkuu huyo kupitisha sera zake katika baraza lale la mawaziri lililogawika.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/AFP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman