Lifahamu kundi la Boko Haram
16 Desemba 2020Kundi la itikadi kali la Boko Haram linakiri kuhusika na utekaji wa mamia ya wanafunzi wa kiume katika shule iliyopo jimbo la Katsina kaskazini magharibi mwa Nigeria, hii ikiwa ni kulingana na ujumbe wa sauti kutoka kwa mtu anayejitambulisha kama kiongozi wa vuguvugu hilo.
Kama sauti hiyo ni ya uhakika, shambulizi hilo la Disemba 11 linaashiria kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa ushawishi wake, hadi nje ya ngome yake iliyoko eneo la kaskazini mashariki, wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema.
Unalifahamu vipi kundi hili la Boko Haram? Fuatana nami.
ASILI YA BOKO HARAM
Jina la kundi hilo ambalo ni la kabila ya Hausa linamaanisha "Elimu ya magharibi hairuhusiwi". Lugha ya Hausa inazungumzwa eneo lote la kaskazini mwa Nigeria.
Kwa asili wafuasi wake walikuwa ni wale waliokuwa chini ya mhubiri wa kijeshi Mohammed Yusuf ambaye makao yake yalikuwa kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno na aliyetaka matumizi mapana ya sharia ya Kiislamu kwenye taifa hilo lenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika.
Alifariki dunia akiwa anashikiliwa mahabusu mwaka 2009. Mwaka uliofuata, makamu wake Abubakar Shekau alitangaza kupitia video kwamba alikuwa kiongozi mpya wa kundi hilo.
MBINU.
Chini ya uongozi wa Shekau, Boko Haram walifanya mashambulizi ya kujitoa muhanga kwenye makanisa na masoko na kuwateka maelfu ya watu katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Mwaka 2014, Boko Haram ilianza kuidhibiti miji ya eneo hilo na kujaribu kuanzisha utawala wa Kiislamu kwa kutumia sharia.
Mapema mwaka 2015, Boko Haram ililidhibiti eneo kubwa la ardhi katika eneo linalokaribia ukubwa wa Ubelgiji, karibu na ziwa Chad kabla ya kufurushwa kutoka kwenye mengi ya maeneo hayo na vikosi vya Nigeria, Chad, Cameroon na Niger.
Mashambulizi ya mambomu, uporaji na kuwashambulia kwa risasi wanavijiji na wakazi wa miji yaliendelea.
Zaidi ya watu 30,000 wameuawa na milioni 2 wameyakimbia makazi yao tangu kulipoanza uasi wa kundi hilo mwaka 2009, hii ikiwa ni kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, pamoja na jopo la wataalamu lililojikita New York, linaloangazia masuala ya mahusiano ya kimataifa, CFR.
UTEKAJI
Boko Haram iliwateka zaidi ya wasichana 270 waliokuwa wanasoma shule ya Chibok, kaskazini mashariki mwa Nigeria mwaka 2014, katika shambulizi ambalo liliibua ghadhabu kubwa na kuibua kampeni iliyokwenda sambamba na hashtag, BringBackOurGirls.
Takriban nusu ya wasichana hao hadi sasa ama wameokolewa, wamekimbia ama hawajaweza kurudi nyumbani na baadhi yao wanadhaniwa kuwa walikufa wakiwa wanashikiliwa na waasi hao.
Boko Haramu imekwishawateka maelfu ya raia na watu wengine na kutaka kulipwa fidia kwa lengo la kukusanya fedha za kuendeshea mafunzo na kuwasaidia wake za wapiganaji na mahitaji muhimu, mchambuzi wa masuala ya usalama anasema.
MGAWANYIKO
Mwaka 2015, Shekau aliahidi kulitii kundi kubwa kabisa la kigaidi ulimwenguni linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Lakini mwaka uliofuata, lilimtaja mtu mwingine Abu Musab al-Barnawi kama kiongozi wake katika eneo la Afrika Kaskazini. Shekau alipinga hatua hiyo, na kundi hilo likagawanyika mwaka 2016.
Mchambuzi wa masuala ya usalama anasema mgawanyiko huo ulitokana na hatua ya Shekau ya kukataa kukubaliana na maelekezo ya kundi hilo la IS ya kuwalenga wanajeshi wa Nigeria badala ya raia.
MAENEO YA OPERESHENI
Chimbuko la Boko Haram ni kaskazini mashariki mwa Nigeria, lakini limekuwa likifanya mashambulizi ya mabomu na kuwashambulia watu katika mataifa jirani ya Cameroon, Niger na Chad.
Boko Haram huko nyuma halijawahi kukiri kwamba lilifanya mashambulizi yoyote katika eneo la kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Mashirika: RTRE