1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa wa dunia yaanza rasmi Bayern kidedea

23 Agosti 2014

Msimu wa ligi ya mabingwa wa dunia Bundesliga umeanza rasmi jana,(22.08.2014) na kama ilivyotarajiwa mabingwa watetezi wa ligi hiyo , Bayern Munich wamefanikiwa kuibwaga VFL Wolfsburg kwa mabao 2-1.

Bundesliga Bayern München - VFL Wolfsburg Juel Robben
Bayern Munich wakishangiria baoPicha: Getty Images

Pambano hilo lilifanyika katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich jana usiku. Arjen Robben na Thomas Muller ndio waliopeleka furaha kwa mashabiki wa mabingwa hao watetezi Bayern Munich.

Mabingwa hao kutoka jimbo la Bavaria , wakiwakosa nusu ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza , walionesha kiwango cha juu kwa muda mfupi tu katika kipindi cha kwanza lakini ilitosha kuweza kunyakua pointi zote tatu muhimu mwanzoni mwa msimu huu.

Thomas Muller mshambuliaji wa Bayern MunichPicha: Getty Images

Joachim Loew ashuhudia

Kocha wa mabingwa wa dunia Ujerumani, Joachim Loew alikuwapo katika pambano hilo, na kushuhudia Thomas Muller akiujaza wavuni mpira kwa pasi safi aliyomegewa na Arjen Robben katika dakika ya 37 baada ya mshambuliaji huyo wa pembeni kuwatoka walinzi wawili wa Wolfsburg.

Robert Lewandowski akiichezea Bayern kwa mara ya kwanza akitokea DortmundPicha: Getty Images

Robben akaongeza bao la pili dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili, ambapo mshambuliaji wa Croatia Ivica Olic alifanikiwa kupunguza mwanya wa magoli kwa kupachika bao katika dakika ya 52 ya mchezo.

"Kwa kila kocha duniani ushindi ni kitu muhimu sana," Kocha wa Bayern Pep Guardiola amewaambia waandishi habari baada ya mchezo huo. Baada ya kuwa mbele kwa mabao 2-0 hatukuweza kuudhibiti mchezo vizuri na tulikuwa na nguvu kwa muda wa dakika 65-70. Bado tunahitaji muda zaidi.

Guardiola aliendelea kutumia mbinu yake ya kuwatumia walinzi watatu licha ya kutokuwapo kwa wachezaji muhimu katika kikosi chake na alimtumia mlinzi Holger Badstuber ambaye amerejea tena uwanjani baada ya kuumia goti na kukaa nje ya uwanja kwa karibu miaka miwili.

Ivica Olic(kushoto) wa Wolfsburg akipongezwa baada ya kufunga baoPicha: Getty Images

"Tulifanya vizuri licha ya kutocheza na timu hii hapo kabla," mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani Badstuber amewaambia waandishi habari. Katika kipindi cha pili tulipungukiwa nguvu kidogo lakini kwa jumla ulikuwa mwanzo mzuri." Amesema Badstuber.

Ligi inaendelea

Ligi ya mabingwa wa dunia , Bundesliga inaendelea leo jioni (23.08.2014), ambapo makamu bingwa Borrusia Dortmund wanawakaribisha Bayer Leverkusen , na FC Koln iliyopanda daraja msimu huu inaoneshana kazi na Hamburg SV, timu ambayo ilikaribia kuiaga Bundesliga msimu uliopita na kunusurika kwa ncha ya kidole. Hertha BSC Berlin iko nyumbani ikiisubiri Werder Bremen , Eintracht Frankfurt ina miadi na Freiburg na Hannover wataoneshana kazi na Schalke 04. Hoffenheim watakuwa nyumbani kuwasubiri Augsburg, ambapo hapo kesho Jumapili (24.08.2014) itakuwa zamu ya wageni katika ligi hii Paderborn wakiwakaribisha Mainz 05 na kisha Gladbach watakamilisha ratiba ya kuanza kwa ligi ya Bundesliga wiki ya kwanza kwa kuikaribisha Stuttgart.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre
Mhariri: Yusuf ,Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW