1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa wa Ulaya kutifua vumbi tena

23 Februari 2016

Michuano ya Mabingwa wa Soka Ulaya inaendelea jioni hii kuwania nafasi katika robo fainali. Bayern Munich watakuwa wageni wa Juventus mjini Turin, nayo Arsenal inaikaribisha Barcelona ambayo ndio mabingwa wa sasa.

Nyota wa Bayern Munich wakishangiria goli katika mechi ya awali
Nyota wa Bayern Munich wakishangiria goli katika mechi ya awaliPicha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Kocha wa Bayern Munich mhispania Pep Guardiola amepania kulitwaa kombe la mabingwa wa Ulaya kabla ya kuhamia Manchester City mwishoni mwa msimu huu, lakini timu yake inayoandamwa na majeraha itakuwa na mtihani mgumu jioni hii mbele ya Juventus ambayo safu yake ya ulinzi ni mojawapo ya zile zilizo bora kabisa barani Ulaya.

Alipoulizwa na waandishi wa habari Jumatatu ikiwa kushindwa kulichukua kombe hilo akiwa kocha wa Bayern kuchukuliwe kama dosari katika rekodi yake kama mmoja miongoni mwa makocha mahiri kabisa duniani kwa wakati huu, Guardiola amesema hicho hakiwezi kuwa kigezo cha ufanisi wake.

Kocha wa Bayern Munich Pep GuardiolaPicha: Getty Images/Bongarts/L. Baron

''Nikiwa na Barcelona nilishinda kila kitu, kombe baada ya kombe. Hapa nilitaka kujaribu changamoto mpya, na nitabadilisha tena. Maisha hayaishii katika soka'', amesema Guardiola katika mahojiano hayo.

Mgogoro wa majeraha

Bayern imesafiri bila mabeki wake muhimu Jerome Boateng, Javi Martinez na Holger Badstuber ambao wote wanauguza majeraha tofauti.

Guardiola amesema atategemea kikosi chake cha mashambulizi, na kuipanga timu yake vyema ili iepuke kupoteza mpira ovyo ovyo.

Hata hivyo Juventus ambayo mwaka jana ilifungwa na Barcelona katika mechi ya fainali ya michuano hii ya Mabingwa wa Ulaya, sio timu kibonde ya kubeza. Inaingia katika mchuano huu baada ya mfululizo wa matokeo mazuri katika ligi ya nyumbani. Katika mechi 14 zilizopita, imeshinda 13 na kutoka sare mara moja.

Arsenal katika mtihani

Mechi kati ya Arsenal na Barcelona itakayopigwa katika uwanja wa Emirates inasubiriwa kwa hamu kubwa ya mashabiki wa soko. Ukiondoa mashabiki wa Arsenal ambao kiroho kinawadunda, wapenzi wa soka wanataka kuona maajabu ya Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar, wakiendelea njama ya maangamizi dhidi ya timu pinzani kama ambavyo wamekuwa wakifanya msimu mzima.

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger amesema timu yake itatakiwa kujizatiti kuizui BarcelonaPicha: Getty Images/AFP/I. Kington

Kocha wa Barceloa Luis Enrique amesema hana haja ya kuwaambia chochote washambuliaji hao. ''Chochote kila ambacho ningewata kufanya tayari wanakifanya. Ni raha sana kuwa na vijana hawa kama washambuliaji wa timu yako''. Ametamba Enrique.

Arsene Wenger ambaye timu yake, Arsenal imeshindwa kuvuka kiunzi cha timu 16 za mwisho mara tano mfululizo, amewataka vijana wake kujikakamua na kuliondoa jinamizi hilo kwa kuikandika Barcelona.

Lionel Messi, kama kawaida akiwa tayari kuiongoza Barcelona dimbaniPicha: Getty Images/P. Schmidli

''Itatubidi kupata uwiano katika ya mashambulizi na ulinzi. Tunapaswa kujizatiti, la sivyo tutakabiliwa na mlima mrefu wa kupata katika mechi ya marudio'', amesema Wenger.

Uhondo wa Champions League utaendelea kesho Jumatano, ambapo Manchester City ya Uingereza itakuwa mgeni wa Dynamo Kiev nchini Ukraine. Katika Mechi nyingine ya Jumatano PSV Eindhoven ya Uholanzi itaikaribisha Atletico Madrid ya Uhispania.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, ape,rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman