1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya Premier kuanza tena Juni 17

28 Mei 2020

Kindumbwendumbwe cha ligi kuu ya soka nchini England kiko mbioni kuanza tena Juni 17 baada ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo Jumatano (27.06.2020) kuridhia mpango wa kuanza mazoezi ya pamoja.

Großbritannien Fußball | Premier League | FC Watford vs. FC Liverpool
Picha: Reuters/Action Images

Huko nchini England kindumbwedumbwe cha ligi kuu ya soka kiko mbioni kuanza tena mwezi ujao baada ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo siku ya Jumatano tarehe 27.05.2020 kuridhia mpango wa kuanza mazoezi ya pamoja hata kama baadhi ya wachezaji watakuwa na wasiwasi kuhusiana na kurejea tena dimbani wakati huu wa mlipuko wa janga la virusi vya corona.

Hatua ya kura zilizopigwa na vilabu vya soka 20 ilikuja baada ya kupata kibali kutoka serikalini kwa wachezaji kufanya mazoezi ya pamoja kama timu ikiwa ni kuondolewa kwa vizuizi vya watu kutokukusanyika nchini England.

Wachezaji pamoja na wafanyakazi wa vilabu wamekuwa wakifanyiwa vipimo vya ugonjwa wa Covid 19 mara mbili kwa wiki. Wachezaji wanne kutoka vilabu vitatu katika ligi ya Premier wamefanyiwa vipimo na kukutwa na maambukizi ya virusi vya corona katika vipimo vya wachezaji na wafanyakazi 1,008 wa vilabu siku ya Jumatatu na Jumanne.
Vilabu vya soka nchini humo vitakuwa na mkutano kwa njia ya simu siku ya Jumatano kwa ajili ya kujadili mipango ya kuanza tena nusu ya msimu wa ligi kuu ya kandanda nchini England ikiwa ni pamoja na upangaji wa ratiba ya mechi ambazo zitapigwa bila mashabiki uwanjani. Suala kuhusu eneo la mechi bado halijatatuliwa baada ya vilabu kukataa mapendekezo kwa ratiba zote kuchezwa katika viwanja huru.

Darren Fletcher, mchezaji wa kikosi cha Manchester United.Picha: picture-alliance/dpa/EPA/L. Parnaby

Vilabu pia vinajadili hitaji muhimu la kurejesha pesa za matangazo dola za Kimarekani milioni 400 kwa sababu ya usumbufu katika msimu na mabadiliko ya bidhaa ikiwa ligi hiyo itaanza tena.

Bado kuna dharura zinaandaliwa ikiwa kuna haja ya kuachana na msimu, ambao ulisimamishwa mwezi Machi huku timu ya Liverpool ikiongoza katika msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na alama 25 na michezo tisa ikiwa imebaki.

Kwa sasa, timu zinajaribu kuwaweka katika hali ya kimchezo wachezaji wake baada ya hali isiyo ya kawaida ya kuwaweka nje ya mchezo kufuatia mlipuko wa janga la virusi vya Corona. Baada ya kufanya mazoezi katika vikundi vidogo na kuzuia kusogeleana tangu kuanza tena kwa mazoezi wiki iliyopita, wachezaji wanaweza sasa kuingia katika hatua inayofuata juu ya maandalizi ya michezo.

Itifaki bado inasisitiza sheria ya kutokusogeleana katika shughuli za kijamii ili kuepusha uwezekano wa maambukizi mapya ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid 19. "Vikosi vya timu sasa vinaweza kuanza mazoezi kwa pamoja na kushiriki katika kukabiliana wakati tunapunguza msogeleano wowote wa karibu usiostahili," ilisema taarifa ya ligi kuu ya England.

Ngolo Kante, miongoni mwa wachezaji mahiri wa Chelsea.Picha: Imago Images/Action Plus

England na Uhispania zachukua uzoefu kwa Ujerumani

Wakati ligi kuu ya kandanda ya England ikitarania kuchanja mbuga mwezi ujao Juni 17, ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga ilikwishaanza tangu Mei 16 na wakati huko nchini Uhispania serikali nchini humo imetoa idhini ya kuanza kwa ligi kuu ya soka La Liga hapo Juni 8.

Lionel Messi wa Barceleona katika La liga ya Uhispania.Picha: Imago Images/AFLOSPORT

"Majadiliano yanaendelea wakati kazi ikiendelea kuelekea kuanza tena kwa msimu," ilisema taarifa ya bodi ya ligi kuu.

Katika mzunguko wa nne wa vipimo vya COVID 19 baadaye wiki hii, idadi inayopatikana kwa kila timu itaongezeka hadi 60.

Mlinda lango wa timu ya Bournemouth Aaron Ramsdale na mlinzi wa timu ya Watford Adrian Mariappa ndio wachezaji pekee waliotangazwa kukutwa na ugonjwa wa Covid 19 katika vipimo vya wiki iliyopita. "Sijisikii kuvutiwa kurejea kwa ligi kuu, kwa maana kwamba sio kila mtu yuko sawa nayo," alisema mlinda lango namba mbili wa Watford Heurelho Gomes katika mahojiano ya video. "Ninaamini virusi haviendi mbali kutoka siku moja kwenda nyingine. Kwa kweli tunatumai inafanya hivyo, lakini shida itabaki hadi chanjo itakapopatikana.''

Nabodha wa timu ya Watford Troy Deeney hakurejea mazoezini wiki iliyopita kufuatia wasiwasi juu ya hali ya afya ya mtoto wake.

"Wachezaji wengine wanahitaji muda zaidi, na hiyo inaweza kuwa mbaya kwa vilabu vingine vidogo kwani havina nafasi nyingi," alisema Gomes. "Tunapaswa kurudi tu wakati kila mtu yuko mwema juu yake na tunao wakati zaidi wa kufanya mazoezi na kuzoea."

Na Deo Kaji Makomba

(ape)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW