1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lijue tatizo la kushuka kwa kizazi na madhara yake

19 Julai 2018

Zaidi ya asilimia hamsini ya wanawake walio wahi kuzaa wanatajwa kukabiliwa na tatizo la kushuka kwa kizazi, ambalo limefumbatwa na ufaragha mkubwa hasa katika mataifa yanayoendelea.

Tansania CCBRT Hospital
Madaktari katika hospitali ya CCBRT wakiendelea na upasuaji wa kurudisha kizazi kilichoshuka.Picha: DW/H. Bihoga

Asilimia kubwa ya wanawake ambao hupatwa na tatizo la kushuka kwa kizazi, hutalikiwa na waume zao ama hutelekezwa, huku wananume wengi wakiamini kuwa tatizo hilo linatokana na laana ambayo mwanamke hupata kutoka kwenye mizimu.

 Rhobi Chacha alimwambia mwandishi wa DW kuwa ilimlazimu kutoroka kwa mumewe ili akapate tiba kwa waganga wa kienyeji lakini hakuambulia kitu na badala yake amekaa na tatizo hilo kwa zaidi ya miaka kumi huku hajui watoto wake walipo,

"Sikutaka ile aibu ya kukimbiwa na bwana yangu sababu ya hii nyama sehemu za siri, alie nizalisha aliniambia hii ni laana sababu nilifululiza kuzaa wanawake tu,” alisema mama huyo katika mahojiano na DW.

Idadi ya wananwake kama Rhobi katika mataifa yanayoendelea wanatajwa kuathirika zaidi hasa katika maeneo ya vijijini, ambapo elimu juu ya afya ya uzazi bado ni haba huku ikigubikwa na imani nyingi ambazo haziendani na ushahidi wa kisayansi.

Kushuka kwa kizazi kitaalamu

Nyonga ya mamalia imeumbwa kwa mifupa madhubuti na nyama ambazo zinazunguka kiuno, nyonga imehifadhi viungo mbalimbali vya muhimu ikiwemo kizazi, kibofu cha mkojo pamoja na muishilio wa utumbo mkubwa.

Katika nyonga kuna kitu mithiri ya sakafu iliyotengenezwa kwa misuli, kazi yake kubwa ni kutenganisha sehemu ya juu na chini, upande wa juu ukiwa umehifadhiwa viungo mbalimbali kama kibofu cha mkojo pamoja na kizazi huku upande wa chini ukihifadhi uke pamoja na njia ya haja kubwa.

Wakina mama wodini katika hispitali ya CCBRT ambao wamefanyiwa matibabu na wengine wakisubiri matibabu ya kushuka kwa kizazi.Picha: DW/H. Bihoga

Inapotokea mushkeri katika sakafu hiyo ilioundwa kwa misuli itayosababisha hitilafu mbalimbali ambapo matokeo yake ni kulegea kwa misuli hiyo basi viungo vilivyo kwenye nyonga vinaweza kushuka ikiwemo kizazi, kibofu cha mkojo, ama utumbo wa njia ya haja kubwa au vyote kwa pamoja. Daktari James Chapa wa hospitali ya CCBRT anasema kuwa kushukwa kwa kizazi kunatofautiana

"Wapo wananwake ambao shingo ya kizazi tu ndio inachuka lakini wapo wengine ambao hushuka kizazi chote, na kinashuka kwa namna tofauti kinaweza kushuka kuishia ndani ukeni au kikashuka hadi nje kabisa ya uke”

Sababu za kushuka kwa kizazi

Katika hili wataalamu bingwa wa magonjwa ya wanawake wanathibitisha kuwa tatizo la kushuka kwa kizazi pia linaweza kusababishwa endapo mgonjwa atakuwa anatoa haja kubwa ilio kavu kuliko kawaida, itamlazimu kuisukuma kwa nguvu zaidi ambapo matokeo yake ni misuli ya nyonga kupata mkandamizo, unaosababisha misuli hiyo kulegea na hatimaye huenda kizazi kikashuka.

Kikohozi cha muda mrefu kisichopata tiba kinaweza kusababisha pia mtu kushuka kwa kizazi, kadhalika kunyanyua vitu vizito kunakojirudia tena kwa muda mrefu kunapeleka msukumo wa kishindo katika nyonga ambapo huenda misuli ikalegea na viungo kushuka ikiwemo kizazi.

Kushuka kwa kizazi si tu kwa wananwake ambao tayari wamekwsha zaa hata angalau mara moja lakini pia tatizo hili linawakabili hata wale ambao hawajaza kutokana na sababu za kijenetiki.

"Wapo ambao wao wamezaliwa na ulegevu wa misuli Kundi hili la watu wapo kwenye hatari kubwa ya kushuka kwa kizazi kutokana na wao kuzaliwa wakiwa tayari wanaulegevu wa misuli” anaongeza dokta chapa katika mahojiano maalum na DW.

Aliongeza kuwa umri kwa kiwango fulani pia huchangia mwananmke kupata tatizo hili, hasa wale ambao wamekoma hedhi kutokana na mwili kushindwa kuzalisha kichocheo cha Estorogeni ambacho kazi yake kubwa ni kuifanya ile misuli iwe imara.

Wagonjwa wenyewe hawalijui tatizo la kushuka kwa kizazi.

Tatizo hili linatajwa kuwakabili wanawake tu,kutokana na maumbile yao ya uzazi yalivyo ni tofauti na wanaume, na baadhi wanapokumbwa na tatizo hili hujikuta wakijifungia kwenye dunia ya peke yao kwa kuogopa aibu na hata kusemwa na kuchukuliwa mifano katika jamii yake.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama CCBRT James Chapa, katika mahojiano maalum na DW.Picha: DW/H. Bihoga

Kwa wanawake walio mijini wao hupata fursa ya kuhudhuria kliniki kipindi cha ujauzito hivyo tahahdhari kama hizi huhabarishwa na wahudumu wa afya lakini Kundi ambalo lipo vijijini ni nadra kupata wasaa kama huu kutokana na baadhi yao hawahudhurii kabisa cliniki au huudhuria chini ya wastani.

"Siku ya tatu tu, baada ya kujifungua nilihisi kama nyama inashuka huku chini, ikiwa yai si yai, kama shingo ya kuku, nikaenda hospitali nikaambiwa kizazi kimeshuka, waliniambia sababu mtoto alikuja kwa kasi sana” alisema sikitu mkazi wa jijini Dar essalaam.

Hellena ambae alipata  tatizo hilo wakati anajifungua mtoto wake wa sita miaka ishirini iliopita anasema kuwa, alidumu na uchungu kwa zaidi ya wiki mbili akiwa kwa mkunga wa jadi kijijini kwao Ngara ilimlazimu asubiri hadi mtoto alipotoka  hakuweza kwenda hospitali kupata msaada kwa kuwa ni mbali

"Nilianza kusukuma likawa linatangulia lenyewe hilo linyama, wakawa wanalirudisha kurudi ndani, unajua kichwa cha mtoto unasukuma kwa nguvu kumbe ni lenyewe, nilipata wasiwasi nilidhani litaniulia mtoto, ila baadae walitumia mbinu nikajifungua ila nilichoka sana.”

Hellena kama walivyo watu wengine, alianza kutumia dawa za mitishamba ili kukirudisha ndani lakini haikuwa raisi, maumivu makali aliyapata zaidi pale mumewe alipohitaji kufanya nae tendo la ndoa ilimlazimu kuvumilia maumivu makala ili tu kumridhisha.

"Yaani alikuwa akiingiza tu, unasikia maumivu makali mno hadi machozi yanatoka, ni lazima nifanye sababu je akitoka nje kutafuta wananwake si atapata maradhi ya zinaa, hapana tunaambiwa tuvumilie.”

Madhara ya kushuka kwa kizazi kwa mgonjwa

Madhara ya kifo yanaweza kushuhudiwa kwa mgonjwa ikiwa tu hakuna uzingatiwaji wa matibabu tangu mama apatwe na tatizo hilo, kutokana na kushuka kwa kizazi kunaweza kusababisha kutofanya kazi kwa viungo vingine ikiwemo figo, lakini madhara mengine ni kupata maamukizi kwenye kizazi kutokana na kizazi kuwa nje muda wote.

Baadhi ya wagonjwa wanaokabiliwa na tatizo la kushuka kwa kizazi wengine huzikimbia kabisa ndoa zao na wengine huachwa ama hutelekezwa na waume au wenza wao, hii ni kutokana na tatizo hilo kuhusushwa na imani za kishirikina.

Daktari Adjustus Haule ambae ni mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi wa hospitali ya CCBRT jijini Dar es salaam anansema kuwa, wagonjwa wengi ambao hukumbwa na tatizo hili hujinyanyapaa wenyewe, hawapendi kujichanganya na jamii zao hata watu wao wa karibu kwa kuhofiwa kusemwa vibaya na kutolewa mifano mibaya.

"Tatizo hili wamelifanya kuwa ni la siri sana ndio maana wanajikuta wapo peke yao, wamelihusisha na imani za kishirikina kwakiasi kikubwa, na pia hawapendi kufanya tendo la ndoa kutokana na maumivu makali wanayoyahisi.”

Wahudumu wa afya wakiwa na mwandishi wa DW Dar es Salaam Hawa Bihoga katika chumba cha upasuaji muda mfupi kabla ya kuanza zoezi la upasuaji wa kurudisha kizazi kilichoshuka sehemu yake.Picha: DW/H. Bihoga

Matibabu ya kushuka kwa kizazi

Katika kumsaidia mgonjwa kupata matibabu katika tatizo la kushuka kwa kizazi matibabu yamegawanyika katika makundi miwili wapo ambao watapatiwa tiba ya mazoezi hasa ya nyonga ili kurejesha misuli katika ukakamavu unaotakiwa na mwili na hatimae kizazi kurejea katika sehemu yake.

Kadhalika lipo Kundi la wananwake amabao wanawekewa vifaa maalum ambavyo kitaalamu vinaitwa "Pesars”  ni vimipira maalumu ambavyo vinaukubwa tofauti kulingana na ukubwa wa maumbile ya mgonjwa ambapo kazi kumbwa vinafanya kurudisha kizazi sehemu yake,

Matibabu ya mwisho kabisa yakiwa ni upasuaji na kurekebisha sehemu ambayo inahitilafu ili kumrejeshea mama furaha yake

"Katika upasuaji tunachozingatia ni kama mama amekoma kuzaa basi tunatoa kabisa kizazi, lakini kama bado yupo kwenye rika la kuzaa tunazingatia kurudisha kizazi katika eneo lake linalostahili kukaa na atarudi kama zamani.”

kinga dhidi ya kushuka kwa kizazi

hakuna budi jamii kwa ujumla wake kuzingatia kikamilifu mfumo bora wa maisha, hasa uraibuambao unaweza kuepukika ikiwemo matumizi ya sigara ambayo huenda yakasababisha kikohozi cha muda mrefu

Kupunguza unyanyuaji wa vitu vizito kwa wananwake ambapo kutamuweka salama dhidi ya mkandamizo ambao mwili utauwelekeza kwenye nyonga na kusababisha kulegea kwa misuli ya nyonga.

Mwandishi: Hawa Bihoga - DW, Dar es Salaam

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW