Lissu aibuka na mbinu mpya ya kufanya kampeni
8 Oktoba 2020Lissu kwa sasa harusiwi kufanya kampeni yoyote ya urais kwa kipindi cha siku saba baada ya kamati ya maadili ya tume ya taifa ya uchaguzi kumtia hatiani kutokana na matamshi yake aliyoyatoa kwenye mikutano yake. Ni kama vile anajaribu kuuthibitisha ule msemo kwamba: "Mlango mmoja ukifungwa, mingine kumi huwa wazi!" Mwanasiasa huyo, ambaye kitaalamu ni mwanasheria, amekuja na mbinu mpya ya kuendelea kuonekana hadharani akijishughulisha na mambo mbalimbali ya kijamii, ikiwemo kwenda sokoni kununua mahitaji yake kama vyakula na kusafiri kwenye usafiri wa umma akichanganyika na watu. Soma pia: Lissu asema ziara hiyo haina uhusiano na kampeni za uchaguzi
Licha kwamba kwenye maeneo hayo hafanyi kampeni, lakini hatua yake hiyo inatajwa kuwa mbinu ya kisiasa inayomfanya kuwa karibu zaidi na na wananchi. Kila anakopita hadharani akifanya shughuli zake binafsi, amekuwa akiamsha hisia kubwa za wafuasi wake, ambao baadhi hulazimika kukatiza shughuli zao na kwenda kumshangilia:
Mbali ya kwenda sokoni kupata mahitaji yake, Lissu pia ameonekana kwenye maeneo mengine ya wazi kama vile kutumia usafiri wa umma maarufu kama mabasi ya mwendokasi huku akionekana kupiga soga na abiria wenzake:
Matukio hayo anayafanya baada ya kukamilisha ziara ya mkoani Pwani alikokutana na wanachama wa chama chake na kufanya majadiliano ya ndani. Hata hivyo, ziara hiyo ilizusha mvutano mkubwa na jeshi la polisi waliozuia msafara wake kwa takribani masaa manane. Soma pia: Chadema: Utafiti unaomuweka Magufuli kifua mbele ni propaganda
Wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanasema kwamba Lissu anaonekana kuzichanga vyema karata zake hasa wakati ambako harusiwi kupanda kwenye majukwaa ya kampeni kwa kipindi cha siku saba.
Akiutizama mwenendo huo wa Lissu, mwanasiasa wa siku nyingi na mchambuzi wa masuala ya siasa, Samy Ruhuza, anasema kuwa mgombea huyo anajua anachokifanya na kwa kufanya hivyo anazidi kujiimarisha kisiasa:
Wakati Lissu akiendelea kutumikia kifungo cha wiki moja, mgombea wake mwenza, Salumu Mwalimu, anaendelea kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya nchi kunadi sera za chama chake, na kwa kufanya hivyo kumuombea kura bosi wake na chama chake. Wengi wanajiuliza endapo kweli ni rahisi kumzuwia mgombea kufanya kampeni katika mazingira haya!
George Njogopa/DW Dar es Salaam