Tundu Lissu Mwenyekiti mpya CHADEMA
22 Januari 2025Freeman Mbowe, ambaye amekuwa mwenyekiti wa CHADEMA kwa kipindi cha miongo miwili, alimpongeza mrithi wake, Naibu Mwenyekiti wa zamani, Tundu Lissu, siku ya Jumatano.
"Ninawapongeza Mheshimiwa Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kubeba jukumu la uongozi wa chama,” aliandika Mbowe kupitia mtandao wa X.
Mabadiliko haya yanakuja katikati ya msako mkali dhidi ya upinzani nchini humo na pia migogoro ya ndani ya chama cha CHADEMA, ambayo wachambuzi wanasema inaweza kudhoofisha nafasi yake katika uchaguzi.
Mkutano Mkuu wa chama, ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano kumchagua mwenyekiti, ulianza Jumanne na kuendelea hadi usiku wa manane.
Lissu, aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2020, alimlaumu Mbowe kwa kukaa madarakani muda mrefu na akaahidi kufanya mageuzi ndani ya chama.
Kwa taaluma, Lissu ni mwanasheria, na aliwahi kuwa mbunge kuanzia mwaka 2010 hadi 2017, aliponusurika jaribio la kuuawa.
Tishio la Chadema kuzuwia uchaguzi
Siku ya Jumapili, Rais Samia Suluhu Hassan aliteuliwa bila kupingwa kuwa mgombea urais wa chama tawala CCM.
Soma pia: Wawania uongozi CHADEMA ruksa kuchukua fomu
Aliingia madarakani mwaka 2021 baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake John Magufuli, ambaye alikuwa na mielekeo ya kiimla.
Awali alipongezwa kwa kulegeza masharti dhidi ya upinzani na vyombo vya habari katika nchi yenye takriban watu milioni 67.
Hata hivyo, makundi ya haki za binadamu na serikali za Magharibi zimeikosoa serikali kwa kile wanachokiita kurejea kwa ukandamizaji, ikiwemo kukamatwa kwa wanasiasa wa CHADEMA na matukio ya utekaji na mauaji ya wanaharakati wa upinzani.
Mwezi uliopita, Lissu alionya kwamba chama kingejaribu "kuzuia uchaguzi kwa njia ya makabailiano” endapo mfumo wa uchaguzi usingefanyiwa mageuzi.
Matakwa yake hayo yamepuuzwa kwa muda mrefu na chama tawala.
Abel Kinyondo, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alionya kwamba "migogoro ya ndani ya CHADEMA ya karibuni inahatarisha kuwakatisha tamaa wapiga kura.”
"Nadhani wanahitaji kupanga upya mikakati yao baada ya uchaguzi,” aliongeza.
Mpaka sasa, CHADEMA haijatangaza mgombea wake kwa ajili ya uchaguzi wa urais mwaka huu.