1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msafara wa Tundu Lissu wazuiliwa na jeshi la polisi

6 Oktoba 2020

Msafara wa mgombea urais wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, Tundu Lissu umezuiliwa na jeshi la polisi waliokuwa na silaha wakati mwanasiasa huyo akiwa safarini kuelekea eneo la Kibaha

Tansania | Oppositionsführer Tundu Lissu
Picha: Eric Boniphace/DW

Lissu amesema ziara hiyo ilikuwa haina uhusiano na kampeni za uchaguzi. 

Tundu Lissu ambaye kampeni zake zimesimamishwa kwa muda wa siku saba na kamati ya maadili ya tume ya taifa ya uchaguzi amedai kuwa alikuwa akielekea eneo la kibaha kwa ajili ya kukagua shughuli za chama chake.

Amesisitiza kuwa, ziara hiyo haina uhusiano wowote na mikutano ya kampeni na amefanya hivyo kama hatua ya kuimarisha shughuli za chama ikiwamo kufanya vikao vya ndani.

Chama chake mwishoni mwa wiki kiliridhia adhabu aliyopewa mwanasiasa huyo na kikisema kingempangia majukumu mengine wakati huu anapoendelea kutumikia adhabu hiyo ya siku saba.

Chadema yasema kimeridhia adhabu aliyopewa mwanasiasa huyo

Wajumbe wa Chadema wakiwa katika mkutano Dar es SalaamPicha: DW/S. Khamis

Msafara wa Lissu ukiwa na magari yasiyozidi matatu ulizuiliwa katika eneo la Kiluvya nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, na mwenyewe amesisitiza kuwa ataendelea kukaa hapo hadi pale atakapoambiwa sababu ya kuzuiliwa kwake.

Juhudi za kuwapa maafisa wa polisi kuelezea tukio hilo hazikuzaa matunda, na hadi tunakwenda mitamboni mwanasiasa huyo aliendelea kusisitiza kubakia eneo la tukio na hata ikiwezekana kwa siku kadhaa.

Katika hatua nyingine, wagombea wa urais pamoja na wabunge wameendelea kuzunguka huku na kule wakiwafikia wapiga kura kwa kunadi sera zao.

Mgombea urais wa chama cha wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba mbali ya kuendelea kukosoa sera za chama tawala, kadhalika amewasihi wapiga kura kukichagua chama chake kwa lengo la kuzitafutia majawabu kero zinazowaandama.

Chama tawala mbali ya mgombea urais na makamu wake kupanda majukuwaani kunadi sera zake, pia kimekuwa kikiwatumia baadhi ya makada zake wanaoendelea kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya nchi kuzungumza na wapigakura.

 

Mwandishi: George Njogopa