1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lissu: Ninawania nafasi ya mwenyekiti wa CHADEMA

12 Desemba 2024

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu ametangaza nia ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu
Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu.Picha: Eric Boniface

Akizungumza na wanahabari leo katika ukumbi wa Mlimani City mjini Dar es Salaam, Tundu Antipas Lissu, amesema anaitaka nafasi hiyo ambayo inashikiliwa na Freeman Mbowe tangu mwaka 2004.

"Ninapenda kuamini kwamba, ninyi wanachama wenzangu mnaamini nina sifa za kutosha za kugombea nafasi ya juu ya uongozi katika chama chetu," amesema Tundu Lissu ambaye kwa sasa ni makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Lissu amesema tayari ameshawasilisha taarifa rasmi wa Katibu Mkuu wa chama hicho ya kuondoa rasmi, kusudio lake la kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti bara, na badala yake ameshawasilisha taarifa rasmi ya kuwania nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa.

Akishangiliwa na mamia ya wafuasi wake waliofurika kwenye ukumbi wa mikutano, Lissu, amesema kumekuwapo na ushawishi kutoka kwa wanachama wa chama hicho wakimtaka yeye awanie nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.

Viongozi wengine waliowahi kushika nafasi ya Uenyekiti Taifa wa CHADEMA ni Edwin Mtei, mwanzilishi wa chama hicho, na baadaye 2002 hadi 2003 Bob Makani, ambaye alishika nafasi hiyo baada ya Mtei na Mbowe, anayeshikilia nafasi hiyo kuanzia 2004 mpaka sasa.

Lissu asema upinzani Tanzania unahitaji mbinu mpya 

Tundu Lissu akiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.Picha: Eric Boniface/DW

Lissu amesema mbele ya hadhira hiyo kuwa mabadiliko hayo ya uongozi wa juu wa chama yalifanyika kwa mujibu wa katiba ya chama. Akaongeza kuwa CHADEMA hakina budi kuuenzi mfumo wa uongozi ulioanzishwa na waanzilishi wa chama hicho.

Hivi karibuni katika mkutano na wanahabari, Mbowe akijbu maswali kwa wanahabari, alizungumzia kuhusu utata wa nafasi yake ya uenyekiti na kusema wanachama na viongozi wa chama hicho ndiyo watakaoamua agombee au asigombee nafasi hiyo. Mbowe alisisitiza kuwa katiba ya CHADEMA haijamzuia mtu kugombea.

Kadhalika Lissu alitumia fursa hiyo kueleza kuwa mfumo wa utawala wa sasa hauna tofauti na ule uliopita wa hayati John Magufuli na kusema utawala huo unahitaji mbinu tofauti za kuushinda.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW