1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liverpool mabingwa wapya wa Premier League baada ya miaka 30

Sylvia Mwehozi
26 Juni 2020

Liverpool ndio mabingwa wapya wa ligi kuu ya kandanda ya England, na Jürgen Klopp ana mchango mkubwa katika ushindi huo. Hata hivyo mafanikio yake yanaiacha Borussia Dortmund ya Ujerumani ikiwa na kumbukumbu chungu.

England | Jürgen Klopps Manager von Liverpool feiert mit Virgil van Dijk
Picha: picture-alliance/SOLO Syndication/Daily Mail/K. Quigley

Wakati huu ambapo klabu ya Liverpool imetwaa ubingwa wa ligi kuu ya England, tayari kuna uvumi kwamba si muda mrefu ambapo sanamu la Mjerumani Klopp litaonekana katika jiji hilo. Ushindi wa Liverpool unahitimisha ukame wa miaka 30 wa kutotwaa ubingwa wa ligi kuu na kuthibitisha uhusiano wa Klopp na jamii nyingine.

Kaa la moto la uhusiano wake na Dortmund bado linafuka moshi katika mji huo na jinamizi lake limeendelea kuitafutuna klabu hiyo. Ari anayokuwa nayo, furaha yake uwanjani na maisha mapya katika jamii, ndivyo amekuwa akivifanya Klopp katika klabu ya Liverpool na katika taaluma yake; kwanza alipokuwa katika klabu ya Mainz, kisha Dortmund.

Klopp ni mtu mwenye haiba kubwa, mkweli na mwenye kudhihirisha shauku yake kwa uwazi. Hili linamfanya kuwa mtu anayependwa na ukichanganya na mafanikio ya soka ni vigumu kufikiria jambo lingine bora kwa kocha huyo.

Jürgen Klopp kocha wa LiverpoolPicha: picture-alliance/Solo Syndication/K. Quigley

Nani asiyetaka kuwa kama Jürgen?

Alipokuwa Mainz, alijifunza kazi kwa kufanya kila kitu. Aliifikisha klabu hiyo ndogo mahali ambako hata wenyewe hawakuwa na fikra kwamba wangepafikia. Alipoondoka, Klopp alidondosha machozi pale alipowaeleza mashabiki kuwa, "kila kitu nilicho mimi, kila kitu ninachoweza kukifanya ni kwa sababu mliniruhusu kuwa hivyo".

Alipotua Dortmund tabia yake ya kurusha ngumi hewani, kurukaruka na kuwasiliana mara kwa mara na mashabiki kindakindaki wa sehemu ya kusini mwa uwanja maarufu kama "Ukuta wa Njano", vilizusha utata kwa mji huo ambao haukuwa umejiandaa kwa kile ambacho kingetokea.

Alipoikacha klabu hiyo mafanikio ya klabu yalikuwa yakilegalega kiasi fulani, lakini uhusiano wake na klabu pamoja na jamii ya Wana Dortmund ulisalia. Na ndio sababu ya kwa nini alama ya sasa ya Borussia Dortmund unahusishwa na Klopp kama ilivyo kwa Liverpool hivi sasa.

Miaka mitano baada ya Klopp kuondoka Dortmund, kumbukumbu zake zimekuwa kama jinamizi linaloitafuna klabu hiyo. Katika jitihada za kuondokana na jinamizi hilo, klabu hiyo iliamua kuchukua mwelekeo tofauti. Thomas Tuchel alifanikisha Dortmund kushinda kikombe cha Ujerumani, lakini hamasa zilikosekana wazi.

Mashabiki wa Liverpool wakishangilia ubingwa wa klabu yao Picha: picture-alliance/Offside/A. Devlin

Peter Bosz alikuwa meneja mbovu katika wakati ambao pia haukuwa mzuri na ikampasa Peter Stöger kusafisha makosa yake. Chini ya Lucien Favre, Dortmund wamerejea katika ushindani lakini tathmini yake ya mara kwa mara ya wapinzani wake wakati wa mikutano ya waandishi wa habari na aibu yake vinamfanya kutiliwa shaka endapo nafasi hiyo anaimudu.

Uamuzi wa klabu hiyo wa kuwateua makocha wakuu ambao ni tofauti na Klopp unathibitisha kwamba Dortmund hawajaweza kusonga mbele kikamilifu. Wangepaswa kutambua kwamba Dortmund ya 2020 ilitengenezwa na Klopp.

Sifa moja aliyo nayo Klopp ni kwamba anajenga uhusiano katika njia inayowakumbusha umuhimu wa uongozi mzuri sio tu kufahamu mbinu za soka, lakini pia kuwaelewa watu. Anataka kukijua kikosi chake lakini pia jamii yake. Na hayo ndiyo yanakosekana pale anapoondoka kwenye timu. Soka la Ujerumani halijakuwa sawasawa tangu alipoondoka. Borussia Dortmund, imeshindwa kukiri hilo na hivyo Liverpool inapaswa kukumbuka muda utakapofika wa Klopp kuondoka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW