1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liverpool, Madrid kuumana Ligi ya Mabingwa

20 Februari 2023

Uhondo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya unarejea huku kukiwa na mechi tamu tamu ikiwemo ya miamba mawili wa soka la Ulaya Liverpool dhidi ya Real Madrid. Timu hizo kwa pamoja zimeshinda mataji 20 ya Champions League

UEFA Champions League Finale | Liverpool FC vs Real Madrid
Picha: Mustafa Yalcin/AA/picture alliance

Mechi yao ya hatua ya timu 16 katika dimba la Anfield kesho Jumanne pia ni marudio ya fainali ya mwaka jana mjini Paris, ambayo ilishuhudia Madrid ikiweka historia kwa kubeba taji hilo kwa mara ya 14 katika dimba la Stade de France.

Katika mechi nyingine ya kesho, washindi wa Kombe la Ligi ya Europa Eintracht Frankfurt wanaialika timu ambayo ipo katika kiwango bora kabisa barani Ulaya, kutoka Italia, Napoli ambayo inaongoza msimamo wa Serie A na pengo la pointi 15. Napoli inaongozwa na mshambuliaji wa Kinigeria mwenye umri wa miaka 24 Victor Osimhen, ambaye amefunga mabao 19 katika mashindano yote msimu huu. Kwa upande wa Frankfurt, mshambuliaji wa Kifaransa Randal Kolo Muani ndiye anayeibeba timu hiyo.  Ana mabao 15 katika mechi 30 kwa msimu huu.

Jumatano kuna mechi mbili ambapo suali wanalojiuliza Manchester City ni, jee huu ni mwaka wao? Champions League ndilo taji pekee ambalo limewaponyoka tangu waliponunuliwa na mabwenyewe wa Abu Dhabi mwaka wa 2008. Kuwasili kwa Erling Haaland mwaka uliopita kulionekana kubadilisha pakubwa muelekeo wa klabu hiyo isipokuwa bado kuna maswali kuhusu timu hiyo ya Pep Guardiola katika ligi ya Premier. Vijana hao wanapigiwa upatu kushinda mechi yao ya ugenini dhidi ya RB Leipzig nchini Ujerumani.

Nayo Inter Milan, itaialika Porto na kama inahitaji nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo, mengo yatategemea Romelu Lukaku kuwa fit na kuanza kufunga mabao.  Mshindi wa kombe la Dunia Lautaro Martinez amekuwa moto wa kuotewa mbali mbele ya lango tangu aliporejea kutoka kikosi cha Argentina kilichopata mafanikio nchini Qatar, akifunga mabao manane katika mechi zake kumi za mwisho.

reuters