LONDON: Madai ya Annan yakanushwa na Marekani na Uingereza
16 Aprili 2005Marekani na Uingereza zimekanusha madai ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan kuwa nchi hizo zilipuuza,biashara ya magendo ya mafuta iliofanywa na serikali ya Saddam Hussein.Siku ya Alkhamis Annan alisema,Uingereza na Marekani zilijua kuwa mafuta ya Iraq yalikuwa yakisafirishwa Jordan na Uturuki licha ya kuwepo vikwazo vya Umoja wa Mataifa.Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Jack Straw amesema madai hayo "si sahihi".Na Marekani nayo imepuuza madai hayo.Msemaji wa Marekani katika Umoja wa Mataifa,Richard Grenell amesema,Washington haina habari yo yote kuhusu mafuta yaliosafirishwa kwa magendo wakati huo.Annan binafsi pia hivi karibuni alikabiliwa na shinikizo la madai kuwa mwanae wa kiume,alihusika na "Mradi wa kuiruhusu Iraq kuuza mafuta ili iweze kununua chakula".