LONDON: wakaguzi wa afya wazuru kampuni ya utafiti
6 Agosti 2007Wakaguzi wa afya na usalama nchini Uingereza wamezuru kampuni ya utafiti kusini mwa mji wa England kutathmini chanzo cha mkurupuko wa virusi vinavyo sababisha ugonjwa wa miguu na midomo kwa wanyama.
Awali wizara ya mazingira ilithibitisha kwamba virusi hivyo vilivyogunduliwa katika shamba moja la mji wa Surey vimefanana na vile vinavyotumiwa kutengeneza kinga ya ugonjwa huo katika kampuni hiyo ya utafiti iliyo katika eneo la Pirbright. Taarifa kamili itatolewa baada ya uchunguzi kukamilika.
Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amesema juhudi zinafanyika kudhibiti ugonjwa huo na hatimae kuumaliza kabisa.
Kufuatia mkurupuko huo wa ugonjwa wa miguu na midomo nchi za umoja wa ulaya zimepiga marufuku uagizaji wa bidhaa za nyama kutoka Uingereza.
Hapa nchini Ujerumani mashamba matano ya mifugo yamewekewa chini ya kizuizi kama tahadhari kwa kuwa yaliagiza wanyama kutoka Uingereza katika siku za hivi karibuni.